Barua ya Baraza Kuu la CUF kwa Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi Kupinga Msimamo na Ushauri Wake Kuhusu Profesa Lipumba
YAH: MSIMAMO NA USHAURI WA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA KUHUSU UONGOZI WA KITAIFA WA CHAMA CHA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF)
Tafadhali husika na somo hapo juu pamoja na barua yako ya tarehe 23 Septemba 2016 yenye Kumb Na. HA.322/362/14/85 kuhusu somo tajwa.
Baraza Kuu la Uongozi la The Civic United Front (CUF) – Chama Cha Wananchi, kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu wa Chama, limepokea barua yako tajwa hapo juu pamoja na taarifa fupi inayoainisha msimamo na ushauri wa Msajili wa Vyama vya Siasa kwa Chama cha The Civic United Front (CUF) na kuijadili kwa kina. Yafuatayo ni majibu na msimamo wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF ambayo tunapenda kuyawasilisha ili ofisi yako iyafanyie kazi.
Awali ya yote, tunakupongeza kwa namna ulivyofuatilia kwa kina, kupitia wadhifa wako kama Msajili wa Vyama Vya Siasa Tanzania, malalamiko yaliyowasilishwa kwako na watu uliowatambua kwenye taarifa yako fupi.
Aidha, tumebaini kuwa ofisi yako imejikita katika kutoa tafsiri ya Katiba ya Chama cha The Civic United Front (CUF) toleo la mwaka 2014 pamoja na tafsiri ya matukio na maamuzi ya vikao vya Chama kwa mujibu wa ufahamu wako.
Pili, tumebaini kuwa ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa haina mamlaka ya kisheria kutoa “Msimamo na Muongozo” kwa chama cha siasa kilichosajiliwa nchini Tanzania.
Majukumu ya ofisi yako kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha ofisi yako, Sheria ya Vyama Vya Siasa Sura ya 258, haikupi mamlaka ya kutoa msimamo na Muongozo.
Badala yake, unapewa mamlaka ya kuhifadhi kumbukumbu na taarifa za vyama vya siasa. Majibu haya yanatokana na ukweli kuwa ofisi yako imewahi kuonywa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam katika shauri la Madai Na. 6 la mwaka 2003 baina ya Emmanuel Nyenyemela and Another Versus Registrar of Political Parties and Others mbele ya Mheshimiwa Jaji Mihayo. Mahakama ilieleza kama ifuatavyo kwenye ukurasa wa pili wa hukumu:
“In the same vein, I do not see anywhere in the Political Parties Act where the Registrar has power to bless or condemn meetings of political parties or decisions that they make”. (Katika Muktadha huo huo sioni mahali popote kwenye Sheria ya Vyama vya Siasa ambapo Msajili wa Vyama ana mamlaka ya kubariki au kupinga vikao vya vyama vya suasa au maamuzi yanayofanywa na vikao hivyo).
Tunapenda utambue kuwa uamuzi na muongozo huo wa Mahakama Kuu ya Tanzania haukuwahi kutenguliwa na Mahakama yoyote ile na hivyo tunaamini wewe ukiwa na weledi katika taaluma ya sheria na Jaji wa Mahakama kuu, unafahamu uamuzi huo na namna ya kuutumia.
Tatu, pamoja na kubaini yaliyomo kwenye aya zilizotangulia hapo juu, tunapenda upokee majibu yetu kuhusiana na kila kipengele ulichoongelea kwenye Taarifa yako fupi kama ifuatavyo:
1. MAMLAKA NA WAJIBU WA MSAJILI KUSHUGHULIKIA MGOGORO HUU
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF linasikitika na upotoshaji wa makusudi uliofanywa na ofisi yako kuhusu tafsiri ya vifungu vya Sheria ya Vyama Vya siasa, Sura ya 258 ulivyovitaja katika ukurasa wa pili wa Taarifa yako fupi ili kujipa mamlaka ya kushughulikia kile ulichokiita mgogoro wa Uongozi katika Chama chetu.
Tunapenda urejee vifungu ulivyotumia ambavyo tunavichapisha tena hapa chini:
Kifungu cha “8A (1) There shall be a Registrar of Political Parties into which names, addresses, and other particulars of Registered Political Parties or national leaders of Political Parties shall be entered.” (Kutakuwa na Msajili wa Vyama vya Siasa ambako majina, anwani na taarifa zingine za Vyama vya Siasa vilivyosajiliwa au viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa zitawekwa).
Kifungu cha 10(f) “No Political Party shall be qualified to be fully registered unless …..(a)…….(e) (Hakuna Chama cha siasa kitakachofaulu kupewa usajili wa kudumu hadi……)
(f) it has submitted the names of the national leadership of the party and such leadership draws its members from both Tanzania Zanzibar and Mainland Tanzania, and” (kiwe kimewasilisha majina ya uongozi wa kitaifa na uongozi wa chama hicho uundwe na wanachama kutoka Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara, na)
Ukivisoma vifungu hivyo hapo juu, katika sheria tajwa, utabaini kuwa havina kabisa uhusiano na kukupa wewe mamlaka au wajibu wa kuchunguza na kujiridhisha kuhusu usahihi wa mabadiliko katika uongozi wa Kitaifa wa Chama na ama kutengua au kubariki maamuzi halali ya vikao halali vya chama chochote. Zingatia pia hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania ambayo tayari tumeitaja hapo juu. Tumejiridhisha kuwa mamlaka uliyojitwisha hayakuwa yako na pia hukuyatenda kwa kuzingatia misingi ya haki.
2. KUJIUZULU KWA PROFESA IBRAHIM LIPUMBA NA KUTENGUA BARUA YAKE YA KUJIUZULU
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF linatambua kuwa Chama cha The Civic United Front (CUF) kinaongozwa na Katiba yake halali, toleo la mwaka 2014. Tunapenda utambue kuwa kujiuzulu kwa kiongozi ni wakati wowote kwa mujibu wa Ibara ya 117(1). Kuhusu utaratibu uliowekwa na ibara ya 117(2) hauathiri haki ya kiongozi kujiuzulu wakati wowote.
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba aliandika barua ya kujiuzulu nafasi ya Mwenyekiti wa CUF Taifa kuanzia tarehe 5/08/2015 ambayo ni siku aliyoandika barua hiyo na aliutangaza uamuzi wake huo mbele ya vyombo vya habari tarehe 6/8/2015.
Katika Barua yake ya kung’atuka wadhifa wa Mwenyekiti wa Taifa wa CUF ilisema ;
”Leo tarehe 5 Agosti 2015 najiuzulu rasmi nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa CUF. Naendelea kuwa Mwanachama na kadi yangu nimeilipia mpaka 2020.”
Prof. Lipumba alitekeleza kujiuzulu kwake bila kusubiri kukubaliwa na Mkutano Mkuu wa Chama kwa mujibu wa Ibara 117(2) ya Katiba ya Chama. Prof. Lipumba alikua na mamlaka ya kuhakikisha kuwa Mkutano Mkuu unaitishwa ili kukubali kujiuzulu kwake lakini hakufanya hivyo.
Kama ulivyoeleza katika taarifa yako, Katiba ya CUF inatambua haki ya kujiuzulu uongozi lakini haizungumzii kutengua uamuzi wa kujiuzulu. Prof Lipumba asingeweza kutengua uamuzi wake wa kujiuzulu kwa sababu alishautekeleza. Na aliacha ofisi na majukumu ya Mwenyekiti wa Taifa wa CUF kwa mujibu wa Ibara ya 91 ya Katiba ya Chama kwa zaidi ya miezi kumi. Kuna msemo “you can not eat a cake and have it.”
Kwa hiyo suala la Prof. Ibrahim Haruna Lipumba kurudi kwenye nafasi ya Mwenyekiti wa CUF Taifa baada ya zaidi ya miezi kumi ni wazo chelewefu (afterthought) na ndiyo maana amekua akiitika wito wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kama Mwalikwa kutoa maoni juu ya mambo mbalimbali.
3) BAADHI YA WAJUMBE WA MKUTANO MKUU MAALUM KUHITAJI PROFESA LIPUMBA AITWE KATIKA CHUMBA CHA MKUTANO KUJIELEZA.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF limesikitishwa kwamba hujajielekeza kabisa juu ya namna Prof. Lipumba alivyovamia Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa tarehe 21/08/2016 akiwa na genge la wahuni ambao sio wajumbe wala waalikwa wa mkutano huo (kama yeye) na wahuni hao wakiwa na silaha mbalimbali na kwa hiyo tunachukulia kwamba unaunga mkono vitendo hivyo.
Ibara ya 117(2) ya Katiba ya CUF haitoi fursa kwa kiongozi aliyejiuzulu kujieleza juu ya kujiuzulu kwake mbele mkutano husika. Hata hivyo, umuhimu huo haukuwepo kwa sababu chama kiliridhika kwamba ni yeye ndiye aliyejiuzulu na aliondoka ofisini na akaacha kutekeleza majukumu yake ya Mwenyekeiti wa CUF Taifa.
Pia alikabidhi barua yake ya kujiuzulu kwa mkono wake mwenyewe tarehe 05/08/2015 na siku iliyofuata ya tarehe 06/08/2015 aliufahamisha umma kupitia vyombo vya habari kwamba alijiuzulu na alithibitisha hiyo. Maelezo ya Profesa Ibrahim Lipumba yalikuwa tayari yanafahamika kwa wajumbe wengi wa Mkutano na hakukuwa na suala jipya kuhusiana na kujiuzulu kwake.
Hivyo haukuwa sahihi hata kidogo kusema kuwa Profesa Lipumba alipaswa kujieleza mbele ya Mkutano Mkuu.
Msimamo wako huo ni kinyume na Katiba ya CUF na hali halisi ilivyokuwa. Mashaka uliyojijengea kuwa huenda barua iliyosomwa haikuwa yake hayana msingi wowote maana tangu mwaka 2015 ofisi yako imekuwa ikifanya kazi na Chama cha CUF kupitia viongozi wengine na ukiwa Mtanzania tunaamini ulipata taarifa za kujiuzulu kwake kwa njia nyingi. Ofisi yako pia ilipokea taarifa rasmi kutoka CUF, kwa hiyo inashangaza sana kusikia kuwa hata ofisi yako haikuwa na taarifa za kujiuzulu kwa Profesa Lipumba.
4). UHALALI WA KURA ZILIZOPIGWA KUKUBALI AU KUKATAA PROFESA LIPUMBA KUJIUZULU.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF linabaini tafsiri ya matumizi ya ibara ya 77(8) (d) ya Katiba ya CUF ambayo tunapenda kuidurusu hapa chini:
“77(8) Kwa madhumuni ya kijifungu cha (7) cha kifungu hiki, maamuzi muhimu ni pamoja na
(d) kuwasimamisha, kuwaachisha au kuwafukuza uongozi na/ au uanachama viongozi wakuu wa Kitaifa wa Chama pamoja na viongozi wengine wa Kitaifa kama ilivyoainishwa ndani ya Katiba hii.”
Kijifungu hicho hakihitaji tafsiri yoyote na kiko wazi, kwamba matumizi ya kifungu hiki ni pale ambapo yanajadiliwa masuala ya kuwasimamisha, kuwaachisha au kuwafukuza uongozi na au uanachama viongozi wakuu wa Kitaifa wa Chama. Katiba hii haitoi wajibu wala haifanyi suala la kujiuzulu Kiongozi wa Kitaifa wa Chama kuwa ni jambo muhimu linalohitaji kupigiwa Kura kwa mujibu wa tafsiri yako. Ikiwa Lipumba angelikuwa anasimamishwa, anaachishwa au kufukuzwa uongozi au uanachama ndipo matakwa ya uamuzi muhimu kikatiba yangelifanyika.
Lakini Profesa Lipumba alijiuzulu mwenyewe, hakusimamishwa, hakuachishwa na wala hakufukuzwa uanachama au uongozi kwa hiyo Mkutano Mkuu wa CUF kikatiba hauwezi kushughulikia suala la kujiuzulu kwa kiongozi kama uamuzi muhimu.
Tambua pia kuwa Katiba ya CUF ni yetu wenyewe na wewe ni Msajili, tunaifahamu vyema sisi wanachama na viongozi kuhusu maudhui yake kuliko wewe ambaye mara zote tunakupa taarifa baada ya maamuzi ya vikao na Katiba hiyo kuwasilishwa kwako kwa usajili tu. Kujiuzulu kwa Profesa Ibrahim Haruna Lipumba kulifanyiwa maamuzi kwa mujibu wa Ibara ya 115(1) ya Katiba ya CUF na siyo ibara ya 77(7).
Kura zilizotakiwa ni zaidi ya nusu tu na siyo 2/3 (theluthi mbili) na kura zilizopigwa kubariki kujiuzulu kwake ni 476 ambazo ni asilimia 70 ya idadi ya wajumbe wote wa Mkutano Mkuu na kwa hiyo maamuzi ya ibara ya 117 (2) yalifanywa kwa uhakika, kikatiba na bila shaka yoyote.
Taarifa za vurugu wakati wa maamuzi siyo ya kweli. Unatambua kuwa vurugu hizo zilitokea baada ya ajenda ya kukubali kujiuzulu kwa Profesa Ibrahim Haruna Lipumba kukubaliwa na ajenda hiyo kufungwa na mkutano kuahirishwa kwa mapumziko na kwamba baada ya mapumziko na wakati mkutano uko kwenye ajenda ya pili ndipo vurugu zilitokea.
Hata hivyo, unatambua kuwa vurugu hizo alizisababisha yeye mwenyewe Prof. Lipumba alipofahamu maamuzi ya Mkutano na wakati wa Kuchagua Mwenyekiti mpya wa kujaza nafasi yake iliyoachwa wazi kwa kujiuzulu.
5). UHALALI WA KIKAO CHA BARAZA KUU LA LA UONGOZI LA TAIFA CHA TAREHE 28 AGOSTI 2016.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF limebaini kuwa ofisi yako imetambua Kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa cha tarehe 28 Agosti 2016. Hatuna mashaka na mtazamo huu kwani ndiyo ukweli.
6). MAMLAKA YA BARAZA KUU LA UONGOZI KUCHUKUA HATUA ZA KINIDHAMU.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF halina mashaka na utambuzi wako wa mamlaka ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya viongozi wa Kitaifa wa Chama.
Tunakushauri kifungu ulichotumia ukisome pamoja na vifungu vingine ambavyo ni Ibara ya 82(1) (m) na 83(1).
7). UTARATIBU WA KUCHUKUA HATUA ZA INIDHAMU.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF linapenda kukufahamisha kuwa taarifa ya Kikao cha dharura ilikuwa sahihi na ajenda ilikuwa inafahamika kwa wajumbe wa Kikao kuwa ni kujadili hujuma. Hata hivyo, tunakanusha tuhuma kuwa Maamuzi muhimu kwa mujibu wa ibara ya 77(8) na 81(4) hayakufanyika kwa kuzingatia matakwa ya 2/3 ya wajumbe.
Utatambua kuwa maamuzi yote ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa yanaweza kufanyika kwa maafikiano au kwa wingi wa kura. Tunakushauri urejee Ibara ya 81 (3) ya Katiba ya chama ambapo hata maamuzi muhimu yanahusika.
Tafsiri ya neno “Unanimously” hayamaanishi “Consensus”. Tunajiridhisha kuwa neno Unanimously kwa muktadha wa Chama chetu ni kuwa wajumbe wote walipiga kura na hakukuwa na mjumbe aliyepinga. Hatukuwahi kupata taarifa za mtu yeyote aliyethibitika kuwa alinyimwa fursa ya kupiga kura. Kama maamuzi yalifanyika unanimously, basi yalifanyika kwa wingi wa wajumbe zaidi ya 2/3 kila upande. Katiba ilizingatiwa.
8. UTEUZI WA VIONGOZI WA KITAIFA ULIOFANYWA NA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF linapenda ufahamu kuwa ibara ya 101 inalipa Baraza Kuu la Uongozi Taifa uwezo wa kuunda Kamati yoyote na hivyo kujumuisha uwezo wa kuunda Kamati ya Uongozi ilipoona kuna haja hiyo. Kamati iliyoundwa ni halali kwa ajili ya utekelezaji mzuri wa sera na itikadi za chama. Majukumu ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Chama Taifa yana lengo la kusaidia utekelezaji mzuri wa sera na itikadi za Chama, kwa hiyo majukumu ni yale yale na siyo tofauti.
Kwa mantiki hiyo, Kamati zote mbili yaani ile ya awali iliyokuwa chini ya Mwenyekiti Mhe. Wakili msomi Twaha Issa Taslima na hii ya sasa iliyo chini ya Mhe. Julius Mtatiro zote ni halali kwa mujibu wa katiba ya Chama. Ofisi yako ilipokea taarifa ya Chama na inayo (ambalo ndilo jukumu lako) iliyokuwa ikikueleza kuundwa kwa Kamati ya Uongozi ya awali iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Mhe. Twaha Taslima ambayo hukuhoji uhalali wake na uliitambua na hata kufanya kazi nayo ilipokuwa ikiwasiliana na wewe. Haiwezekani uone na utambue uhalali wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kuunda Kamati ya Uongozi kwa kipindi cha Agosti 2015 hadi Agosti 2016 lakini usione uhalali wa kuundwa Kamati ya aina hiyo hiyo iliyoundwa tarehe 28 Agosti, 2016.
9. UHALALI WA UTEUZI WA VIONGOZI WA KITAIFA ULIOFANYWA NA KIKAO CHA BARAZA KUU LA TAREHE 28 AGOSTI 2026.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF linapenda kusisitiza kuwa uteuzi ulikuwa halali kama tulivyoeleza hapo juu. Kama ulivyoeleza wewe, utabaini kuwa mamlaka ya uteuzi wa viongozi wa Kitaifa ni Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na ndicho kilichofanyika na ambacho ni msimamo wa Chama. Na hiyo ina maana kuwa msimamo wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF ni kuwa Ndugu. Julius Mtatiro, Ndugu. Severina Mwijage na Ndugu. Katani Katani ndiyo wajumbe wa kamati hiyo ya uongozi na wanatambulika kikatiba katika chama chetu kama Wajumbe wa Kamati ya Uongozi hadi hapo chama kitakapochagua Mwenyekiti mwingine.
10). HITIMISHO
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF limejiridhisha kuwa katika taarifa yako fupi umeweka hitimisho ambalo linatoa hukumu (judgment) badala ya kushauri au kutoa taarifa kama ulivyoitaja.
Kama tulivyokwisha kueleza kwenye utangulizi wa barua yetu na kwa kuzingatia Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258 toleo la mwaka 2015 na kwa kuzingatia hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam, mbele ya Mhe. Jaji Mihayo ambayo tunaiambatanisha na barua hii kwa taarifa, tafadhali tambua kwamba hukumu yako ni batili na haina mashiko kisheria.
Kwa yale ambayo umetoa ushauri kwa mujibu wa Katiba ya Chama chetu, Chama kina hiyari ya kuukubali au kuukataa ushauri huo kwa kuzingatia misingi ya Katiba yake, Kanuni zake na kuhakikisha haki sawa kwa wote inatendeka wakati wote.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF linasisitiza kuwa maamuzi yaliyofanywa na vikao halali vya Chama vya Mkutano Mkuu Maalum wa tarehe 21/08/2016 na Baraza Kuu la Uongozi la Chama Taifa la tarehe 28/08/2016 ni halali na tunakusihi uyatambue hivyo.
Tunakukumbusha na kukukusihi usiruhusu Ofisi yako itumike vibaya kutuletea mitafaruku na migogoro isiyo ya lazima katika Chama chetu na hata kusababisha uvunjifu wa amani kama ilivyotokea Jumamosi, tarehe 24 Septemba, 2016 katika Ofisi Kuu ya chama chetu Buguruni Dar Es Salaam. Ushauri huu unazingatia ukweli kuwa Msajili wa Vyama Vya Siasa Tanzania ni mteule wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa. Nguvu ya Chama cha CUF Tanzania inafahamika na hasa katika ushiriki wake na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka 2015.
Matukio yaliyojitokeza Zanzibar na siasa za nchi hii ni lazima yazingatiwe wakati ukitekeleza majukumu yako ili kuepuka kutumiwa vibaya na watu walioshiriki kuhujumu chama chetu na demokrasia wakati wa uchaguzi mkuu wa 2015 na marudio yake 2016 kwa Zanzibar. Taarifa tulizo nazo za malengo ya Profesa Lipumba kuhujumu siasa za Chama Cha Civic United Front (CUF) na mahusiano ya Chama na taasisi nyingine zinajidhihirisha katika matukio yaliyofanywa na Profesa Lipumba tarehe 21 Agosti 2016 (Ubungo Plaza, Dar Es Salaam – kwenye Mkutano Mkuu Maalum) na tarehe 24 Septemba 2016 (wakati akitekeleza kwa nguvu kile anachokiita “kurudishiwa uenyekiti wake na Msajili) baada ya barua yako tajwa.
Mwisho, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF haliukubali ushauri wako kwa sababu umevuka mipaka ya mamlaka yako uliyokabidhiwa na Sheria namba 5 ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992, imekiuka miongozo ya mhimili wa Mahakama ambayo imekwishatolewa juu ya mamlaka yako na unakiuka misingi ya katiba ambayo inamtaka kila mtu aliyepewa mamlaka katika nchi yetu azingatie sheria za nchi.
Kwa sababu hiyo Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF linakujulisha rasmi kuwa, maamuzi ya vikao halali vya chama kwa maana ya Mkutano Mkuu wa Taifa tarehe 21 Agosti 2016 na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la tarehe 28 Agosti 2016 yanabakia pale pale na kwamba Profesa Lipumba siyo Mwenyekiti wa The Civic United Front CUF Chama Cha Wananchi na kuwa, wanachama na viongozi wote waliosimamishwa na ama kufukuzwa katika kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa cha tarehe 28 Agosti 2016 wanaendelea kuwa chini ya maamuzi hayo hadi pale mchakato wa kikatiba wa kuwasikiliza (kwa waliosimamishwa) utakapokamilika.
Hatua yoyote ile ya kutengua maamuzi yoyote ya vikao halali vya chama chetu itafanywa na vikao husika vya chama au vikao vya juu yake kama ambavyo katiba yetu imeelekeza na kwamba hatutakubali Ofisi yako kutuamulia nani anapaswa kuongoza chama chetu kwa wakati gani ama tujiongoze katika chama chetu kwa namna gani.
Tunawasilisha.
HAKI SAWA KWA WOTE
…………………………………..
MAALIM SEIF SHARIF HAMAD
KATIBU MKUU
NAKALA;
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba
Kilongawima, Kunduchi,
Dar es Salaam.
Bwana Ridhiwani H. Kilala na Wenzako wawili
Bwana Abdul Kambaya na Shashu Lugeye.
Barua ya Baraza Kuu la CUF kwa Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi Kupinga Msimamo na Ushauri Wake Kuhusu Profesa Lipumba
Reviewed by Unknown
on
Oktoba 03, 2016
Rating:
Post a Comment