Header AD

AFYA : KISUKARI NI NINI?(DIABETES MELLITUS)

Kisukari ni nini?Kisukari ni moja ya magonjwa sugu yanayoisumbua jamii. Kisukari hutokana na kiasi cha sukari katika damu kuwa kingi kuliko kawaida. Katika damu kuna chembehai(cells) mbalimbali zenye kazi tofauti kama kusafirisha virutubisho,oksijeni,na nyingine
zina kazi za kupambana na bakteria,virusi nk. Miongoni mwa virutubisho katika damu ni sukari(glucose).
Damu ya mtu mwenye afya njema ina kiasi cha sukari kati ya 82-115mg/dL(hiki ni kipimo maalumu kinachotumiwa kliniki kupima sukari katika damu).

Muhtasari.
Katika mfumo wa chakula kuna kiungo kinachoitwa kongosho(pancreas) ambacho kazi yake ni kuzalisha hormoni iitwayo insulin. Insulin ndiyo inatumika kupunguza kiasi cha sukari katika damu. Sasa inapotokea kongosho inapata madhara ya aina yoyote kama vile maambukizi sugu,majeraha
makubwa kutokana na ajali au upasuaji,kansa n.k hushindwa kuzalisha insulin hivyo kusababisha kisukari. Hata hivyo ni muhimu kujua kuwa si kila mtu mwenye sukari nyingi katika damu basi ana kisukari.
Ili kuepuka makosa kama haya,wataalamu kanuni maalumu zilizothibitishwa kwa vipimo kama vigezo vya kuonyesha mtu ana kisukari,kama ifuatavyo;
  • mtu mwenye njaa akipima sukari katika damu ikawa 126mg/dL au zaidi,
  • mtu aliyeshiba akipima sukari ya damu ikawa 200mg/dL au zaidi,
  • au mtu aliyepimwa wakati wowote akawa na 200mg/dL au zaidi na akawa na dalili za kisukari ambazo nitazielezea hapo baadae.

Aina za Kisukari
Kisukari kimegawanywa katika aina kuu mbili ambazo ni;
  1. Kisukari aina ya kwanza(diabetes mellitus type 1)
  2. Kisukari aina ya pili(diabetes mellitus type 2)
wakati mwingine wataalamu hugawanya kisukari katika aina zaidi ya mbili lakini hapa ni aina hizi pekee ambazo nitazielezea kwani ndo zinaathiri jamii kwa kiwango kikubwa . Nyingine nitazielezea kwa kifupi tu hapo baadae.

Kisukari aina ya kwanza(diabetes mellitus type 1)
Hiki ni kisukari kinachoanza katika umri mdogo kutokana na maradhi yanayojulikana kwa kiingereza kama autoimmune diseases.
Maradhi haya yanatokana na mfumo wa chembehai(cells) zinazopambana na bakteria,virusi na vitu vingine vinavyoleta madhara katika mwili kufanya kazi zaidi za kiwango kinachotakiwa hivyo huanza kuua hadi cells zinazotoa insulin.
Ndio maana huanza katika umri mdogo kwa sababu ni ugonjwa wa kurithi. Watu wengi wenye aina hii ya kisukari mara nyingi ni wale wenye maumbo madogo(wembamba) tofauti na aina ya pili ambayo huwapata hasa watu wanene.
Hata hivyo ikumbukwe pia kuwa hata watu wa miaka kama 30 au 40 wanaweza kupata aina hii ya kisukari. Vilevile ingawa si mara nyingi ila ni muhimu kujua kuwa hata watu wanene pia wanaweza kuugua kisukari aina hii ya kwanza.
Kisukari aina ya pili(diabetes mellitus type 2)
Hii ni aina ya kisukari inayowapata watu wazima lakini pia hata vijana wadogo ingawa si mara nyingi.
Tofauti na aina ya kwanza,hii hutokea pale uwezo wa kongosho kutoa insulin unapokuwa umepungua wakati huo huo kuna chembehai(cells) nyingine –hasa za mafuta(free fatty acids)
kwenye viungo ambazo ambazo huzuia insulin
kufanya kazi yake. Kwa mantiki hii watu wanene ndio wapo katika hatari ya kupata kisukari cha aina hii.
Hata hivyo haimaanishi kuwa watu wembamba hawawezi kupata.
Aina nyingine za kisukari ni;

  • Kisukari cha kipindi cha ujauzito-hii huwapata akina mama wanapokuwa wajawazito au baada ya kujifungua lakini mara nyingi mgonjwa hupona baadae. Aina hii ya kisukari inafanana na ile ya pili niliyoeleza hapo juu. Karibu %2 ya wajawazito hupata aina hii ya kisukari.
  • Kisukari cha ujana(Latent autoimmune diabetes of adults -LADA),ambacho huwapata vijana na sababu zake hazijulikani. Hufanana na aina ile ya kwanza lakini mara nyingi huchanganywa na aina ya pili kwa sababu inatokea baadae kidogo kulinganisha na ile ya kwanza.
Dalili za kisukari
Kabla ya kuelezea dalili za kisukari ni muhimu sana kujua kuwa mtu anaweza kuwa na kisukari kwa miaka mingi lakini asiwe na dalili zozote.Ukiwa na dalili kadhaa kati ya zifuatazo basi ni vyema ukaenda kituo cha afya kufanya uchunguzi.
  1. kuwa na kiu kali ya maji hata kama unakunywa maji vya kutosha au kuwa na hamu ya kula sana,
    kukojoa mkojo mara nyingi ambayo inaambatana na kiu,
  2. kuwa na hali ya uchovu mara nyingi hata kama hufanyi kazi nzito,
  3. kupungua au kuongezeka uzito kwa muda mfupi bila sababu za msingi kama maradhi au mabadiliko ya mlo,
  4. kupata maambukizi ya mara kwa mara hasa katika sehemu za siri(ambazo ni tofauti na magonjwa yanayoambukizwa kwa kujamiana),
  5. kupungua uwezo wa kuona,
  6. kupumua kwa haraka hali ya kuwa hukimbii au kufanya kazi nzito au kupumua kwa haraka kisha taratibu kisha haraka….na kuendelea,
  7. kupata ganzi hasa miguuni au kupungua au kutokusikia maumivu,
  8. vidonda kuchelewa kupona au kutokupona kabisa hasa miguuni.
Sukari inapokuwa nyingi katika damu hufanya damu kuwa nzito hivyo kuharibu kuta za mishipa hasa ile mishipa midogo sana. Mishipa ya damu inayoathiriwa mapema zaidi ni ile ya figo,macho na mishipa ya fahamu. Kwa dalili za mwanzo zinazoashiria kisukari ni;
macho -kupungua uwezo wa kuona,
figo– kukojoa mara kwa mara na kupata kiu kali,
mishipa ya fahamu– ganzi na kupungua kwa hisia ya maumivu(mtu mwenye kisukari anaweza kuwa anaungua moto na asijue ).
AFYA : KISUKARI NI NINI?(DIABETES MELLITUS) AFYA : KISUKARI NI NINI?(DIABETES MELLITUS) Reviewed by Unknown on Januari 23, 2017 Rating: 5

Hakuna maoni

Post AD

Propellerads