Header AD

Daktari Feki Akamatwa Akitoa Huduma Hospitali ya Mnazi Mmoja..!!!


WATU saba, akiwamo mmoja anayedaiwa kuwa daktari bandia, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa madai ya kutengeneza kadi bandia za chanjo ya homa ya manjano na kuziuza kwa watu wanaofika hospitali ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya kupata huduma hiyo.

Chanjo hizo ni zile ambazo hutolewa kwa watu ambao wanasafiri nje ya nchi kama kinga kwa ajili ya homa manjano.

Kamishna wa Kanda hiyo, Simon Sirro, akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alimtaja aliyejifanya daktari kuwa ni mfanyabiashara Salum Natali (47), mkazi wa Chanika Magengeni.

Kamanda Sirro aliwataja watuhumiwa wengine ni walinzi watatu ambao ni Aisha Hassan (29) mkazi wa Vingunguti Mikoroshini, Yakobo Msenga (42) mkazi wa Chanika na Junith Dunstan (23) mkazi wa Kiwalani.

Wengine ni Oliver Bwegege (58) mkazi wa Kigogo Mkwajuni, mjasiriamali Fredy Nyomeye (44) mkazi wa Chang’ombe na fundi umeme Mohamed Bwanga (59) mkazi wa Majohe Gongo la Mboto.

Alisema watu hao walikamatwa Januari 16, mwaka huu majira ya saa 11:00 asubuhi baada ya mtoa taarifa (jina linahifadhiwa) kufika hospitalini hapo na kutakiwa kutoa fedha na mmoja wa watuhumiwa hao ili kupatiwa kadi hiyo ya chanjo ya homa ya manjano.

“Katika mahojiano, watuhumiwa hao walikiri kufanya kosa hilo la kughushi na kutoa kadi hizo za chanjo pasi na mtu kuchomwa sindano yenyewe ya chanjo,” alisema.

Kamishna Sirro alisema Natali alikuwa akijifanya kuwa ni daktari aliyekuwa akiwachoma watu sindano.

Alisema uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea ili kuwabaini washiriki wengine katika mtandao huo wa utoaji wa kadi hizo bandia za chanjo bila kutoa chanjo yenyewe husika.

Katika tukio lingine, watu wawili wanaodaiwa kuwa majambazi wameuawa na polisi baada ya kudaiwa kuhusika kwenye tukio la mauaji Boko Basihaya, jijini Dar es Salaam.

Sirro alisema inadaiwa kuwa watu hao walihusika kwenye kifo cha mlinzi wa duka la pombe (Grocery) aliyetajwa kwa jina la Marwa. Alisema watu hao wanadaiwa kumpiga risasi kichwani mtu huyo na kupora Sh. milioni 1.3.

“Baada ya tukio hilo Jumatatu ya wiki hii polisi walimkamata mwendesha bodaboda, Nathan Mathias akiwa kwenye baa iitwayo PK eneo la Kawe, ambaye alikiri kuhusika na tukio hilo na alimtaja Hamis Daudi mkazi wa Boko njia panda Magereza kushirikiana naye.

“Polisi walifanya upekuzi nyumbani kwa Daudi na kuipata silaha aina ya Shotgun Pump Action yenye namba P. 918884 na TZCAR 76475 ikiwa na risasi mbili,” alisema.

Alisema watuhumiwa hao waliwaeleza polisi kuwa bunduki nyingine wameificha maeneo ya Ununio kwenye mabwawa ya chumvi kando ya Bahari ya Hindi hivyo askari walikwenda nao huko kwa ajili ya kuzichukua.
Daktari Feki Akamatwa Akitoa Huduma Hospitali ya Mnazi Mmoja..!!! Daktari Feki Akamatwa Akitoa Huduma Hospitali ya Mnazi Mmoja..!!! Reviewed by Unknown on Januari 28, 2017 Rating: 5

Hakuna maoni

Post AD

Propellerads