Header AD

JE WAJUA?:Mtu mweusi, "Kiumbe mwenye historia tata"


UTANGULIZI
Wasalaam ndugu zangu,
Naomba watalaamu mnijuze hili swali linalonitatiza kwenye maisha yangu kila siku.
Kama binadamu tumetokea sehemu moja kwanini tuwe na utofauti mkubwa hasa kwenye rangi na maumbile? Kuna nadharia nyingi ambazo zimejaribu kuelezea asili ya binadamu lakini bado kuna vitu vimefichika sana hata sisi tusiweze kuvifahamu.



Kitu cha kukumbukwa ni kwamba tofauti na watu wa Asia,
Sehemu kubwa ya historia ya Afrika na watu weusi imeandikwa na wazungu.
Uchina, India, Uarabuni, Uajemi pamoja na mashariki ya mbali waliandika historia na falsafa ambazo zipo hai mpaka leo. Hasahasa jamii ya Waarabu na Wayahudi wamekuta sehemu kubwa ya historia yao ikitunzwa kwa kiwango kikubwa kwasababu dini za Ukristo na Uislamu ambazo ndizo kubwa hapa duniani zaimeanzia huko.

Lakini ukija hapa kwetu Afrika,
Historia kubwa iliyopo ni ile baada ya ukoloni: Ambayo inamweka mwafrika kama kiumbe asiye na mchango wowote katika dunia hii ya leo. Na hata wasomi mashughuli wenye Asili ya Kiafrika kama Cheikh Anta Diop, Ivan Van Sertima, Frantz Fanon, Rudolph Windsor, Simiyu Wandibba, John Clarke, John Franklin na Walter Rodney walipojaribu kuchapisha maandiko yao kuhusu mtu mweusi katika historia ya leo na ile kabla ya ukoloni walipingwa.

Walipingwa na wazungu,
Lakini kibaya zaidi walipingwa na watu weusi ambao wanaamini kwamba hawa wasomi wanataka kupotosha ukweli ili tu wawafanye Waafrika wajisikie vizuri. (Politically Correct History). Mpaka sasa kuna nadharia kubwa hapa duniani ambazo zimetawala historia ya dunia lakini bado na zenyewe hazina mashiko na hazitoi majibu stahiki yenye kutosheleza.

NADHARIA YA KWANZA
:-MTU MWEUSI NDIYE MJENZI MKUBWA WA USTAARABU HAPA DUNIANI

A: ASILI YA MAJINA YA JAMII ZA WATU NDANI YA NADHARIA.

Kuna maneno ambayo yatatumika hivyo ili kuweka mambo sawa na kutowachanganya wasomaji ngoja nielezee chimbuko lake katika historia. Jambo muhimu kabisa kukumbuka ni kwamba majina mengi ya sehemu, taifa au jamii ya watu fulani mara nyingi hutokana na asili ya eneo lile (kama tabia ya nchi), jina la baba wa jamii ile au mtu aliyekaa katika lile eneo husika. Mfano, taifa la Israeli limetokana na Yakobo ( 2006-1859 K.K) ambaye anaaminika kuwa ndiye Baba wa jamii ya Waebrania: au neno Ethiopia, wanahistoria kama Herodotus wa Ugiriki(484-425 K.K) na Flavius Josephus wa Rumi ( 37-100 B.K) walilitumia kutoka kwenye lugha ya kigiriki "Ethiopos" ambalo linamaanisha mtu ambaye ngozi yake imeungua na jua. Hivyo Basi nchi ya Ethiopia ambayo zamani iliitwa Abyssinia imelichukua neno ambalo linaelezea sifa ya watu wanaokaa nchi hiyo: Au Bara la Ulaya ambalo ni Europe limetokana na jina ambalo linaelezea sifa ya eneo ambalo linahusishwa na mwanamke Europa ambaye kwa lugha ya Kigiriki jina lake lina neno "Eurus" na "ops/op-lopt". Ambapo "Eurus" linamaanisha Pana na "ops/op-lopt" linamaanisha sura au uso. Hivyo Ulaya maana yake uso mpana kwasababu Wagiriki pamoja na watu wa zamani waliamini ni eneo kubwa sana.

Neno Afrika limegubikwa na utata mwingi kama ambavyo historia ya watu wake ilivyogubikwa na utata. Mpaka sasa watu tofauti wamejaribu kuelezea chanzo cheke kila mtu akivutia kwake. Baadhi ya wasomi wameelezea neno Afrika lilitokea baada ya Jemedari wa jeshi la Rumi aitwae Scipio Africanus ambaye alishinda vita dhidi ya Ufalme wa Karthago (Carthage) mnamo mwaka 146 K.K. Ambapo dola la Karthago lilikuwepo sehemu ambapo ipo Tunisia leo, hivyo basi Afrika likapewa jina hilo la huyo jemedari. Wengine wakasema neno la Afrika asili yake ni Kigiriki ambapo neno "Aphrike" linalomaanisha Baridi ndiyo asili yake. Wengine wakasema neno la kilatini "Aprica" linalomaanisha hali ya jua kali ndiyo asili yake. Mwanahistoria wa Kigiriki Leo Africanus alisema Afrika asili yake ni neno "Aphrike" linalomaanisha sehemu yenge baridi kali na ya kutisha. Lakini wasomi wengi wanadai kwamba neno Afrika asili yake ni lugha mbili za Kifonike (Phoenecian) na kilatini. Katika lugha ya Kifonike ambayo ilikuwa ni ya watu walioijenga Karthago neno "Afri" kwao ilikuwa ni Vumbi na neno "Ica" limetoholewa kwenye lugha ya Kilatini kumaanisha Ardhi,nchi. Hivyo basi neno Afrika linamaanisha "Nchi/Ardhi yenye vumbi.

Neno Uarabuni nalo lina asili pana katika muktadha wake. Kwanza kabisa wanahistoria manguli wanalihusisha na maneno ya majigambo ya dola la Kiashuru (Assyria) yaliyoandikwa mwaka 853 K.K. Hili lilitokana na kitendo cha mfalme Shalmanasi kumpiga kivita moja ya machifu wake walioasi. Jina la huyo chifu ni Gindibu Mwarabi. Wanahistoria wengi walitumia kuwaelezea watu wa Shamu ambao walikaa katika ghuba ya Uarabu. Lakini wanahistoria kwa upande mwingine wanahusisha neno "Arabu" na lugha za watu wa mashariki ya kati hasahasa Waebrania. Ambapo ziliezea sifa za neno na watu wenyewe. Neno la Kihebrania "Arav" linamaanisha jangwa, ambapo zaidi zaidi kuna lugha zinawealezea zaidi kama watu wanaohamahama au wafanyabiashara. Ukisoma kwenye Biblia kitabu cha pili cha Mambo ya Nyakati 17: 11 kwenye lugha ya Kihebrania utaona kwa mara ya kwanza linatumika kuwaelezea Waarabu kama jamii ya wafugaji. Lakini kwasababu sehemu kubwa ya Elimu ya dunia ya leo imepata ushawishi kutoka kwa nchi za Kigiriki basi Wanafalsafa na Wanahistoria wa Kigiriki walitumia neno Uarabuni kuelezea sehemu yote ya Rasi ya Uarabuni pamoja na nchi kama Misri.

Neno Ethiopia Wagiriki wamelitoa kwenye neno lao "Ethiopos" ambalo "Aitho" linamaanisha naungua na neno "ops" linaamnisha Uso. Hivyo Ethiopia ni mtu aliyeungua uso kwa maana nyingine ni mtu mweusi, na katika historia ya kale watu walioandika sana kama Herodotus, Appolodorus, Marcellinus na Josephus wanasema kuwa watu weusi walikaa mashariki ya kati, Misri, Sudan, Ethiopia, Visiwa vya bahari ya meditteranea na Afrika Kaskazini. Haya yote yalizungumzwa na wanahistoria katika kikao cha UNESCO ambapo tamati haikufikiwa. Japo kwenye Biblia kitabu cha Yeremia 13:23 Mungu aliuliza kwamba Je, Mkushi/Ethiopia anaweza kubadili rangi yake ya mwili? Hili linathibitisha kwamba katika historia kulikuwa na watu weusi na walikuwa wana mchango mkubwa sana kwenye dunia. Herodotus katika maandishi yake aliwaelezea wanaume weusi "Ethiopians" kama watu warefu, wazuri wa sura na wenye nywele ngumu. Lakini leo kuna nchi ya Ethiopia ambayo watu wake wamijiita hivyo kutokana na mandhari ya kihistoria.

Neno Misri katika historia linaonyesha kutumika kimakosa. Kwanza Katika dunia ya kale Wamisri waliita nchi yao "Kemet" ambalo lilimaanisha ardhi nyeusi ya mto naili na pia eneo la watu weusi. Mwanahistoria Flavius Josephus ndiye aliyeelezea Historia ya Malkia wa Sheba ambaye alienda kumtembelea mfalme Suleimani. Huyu malkia wengi wanamuita Mekeda lakini pia katika lugha ya Amhara kuna kumbukumbu inayotoa jina lake jingine kama Birkis. Daktari wa Historia Windsor Rudolf anasema wafalme wengi japo siyo wote walikuwa na majina zaidi ya moja. Mfano Suleimani alipewa jina Yededia alipozaliwa lakini alipokuwa mkubwa aliapishwa kama Suleimani, au Mtoto wa mfalme Suleimani Menelik wa Kwanza alivyoenda kuapishwa Yerusalem alipewa jina Daudi kama babu yake. Hivyo isichanganye mtu kama Josephus alitumia Mekeda na Wengine wakamuita Birkis.

Tukirudi kwenye neno Misri, Wagiriki walilichanganya na jina la mji mkuu wa Kibiashara Misri kipindi hicho ulioitwa "Thebes" ambapo jina lake la pili uliitwa "Aigyptos" hivyo wafanyabiashara wengi waliuita Aigyptos na hivyo jina likakaa hadi kuitwa Egypt. Mfano wa haya mambo hata leo hii upo, katika historia ya Tanganyika hatujawahi kuwa na kabila la Wahehe lakini kutokana na Wajerumani kukosea kabila la Wahehe likazaliwa mpaka leo hii lipo. Au Sehemu kama Tosa-Maganga mkoani Iringi kumtokana na makosa ya wageni kuandika kile walichokisikia wenyeji wakisema. Hivyo Dola la Kale la Misri liliitwa KEMET (Nchi ya Nile Nyeusi au nchi ya watu weusi)

MUHIMU: Tujifunza kitu muhimu, kwamba katika historia siyo kila mtu ambaye alikuwa ni Mwarabu alikuwa ni mwarabu mweupe wa leo hii, na pia siyo kila Mwafrika alikaa hapa Afrika, tukifika huko mbele tutona jinsi ambavyo kulikuwa na muingiliano mkubwa katika hivi vizazi. Mfano mzuri ni kwamba Misri ya leo hii siyo Misri ya zamani kwasababu imetawaliwa na watu wengi tofauti kwa vizazi vingi. Daktari Ivan Van Sertima anasema kwamba kama ilivyo leo Marekani ambayo ilikuwa nchi ya Wahindi wekundu ndivyo ilivyo leo Misri. Kwamba Wenyeji ambao ni Wahind wekundu ni wachache kuliko wahamiaji kutoka barani Ulaya. Hivyo naomba tuvumiliane maana mwishowe nitaweka kila kitabu nilichokisoma na kukifanyia kazi ili wale wanaopenda kusoma wapitie wenyewe na wachambue kipi ni kweli na kipi siyo ukweli.

B: VIZAZI VYA NUHU.

Vyanzo vikubwa vinavyoelezea kuwepo kwa Nuhu na kwamba vizazi vyote vimetokea kwake ni maandiko ya kidini. Basi Nuhu alikuwa na watoto wa kiume watatu waitwao, Japhet, Shem na Ham. Hawa ndiyo ndiyo mababa wa vizazi vyetu ambavyo vipo leo hapa duniani. Jambo la kuliweka sawa ni kwamba hapo zamani vizazi vilikuwa haviangaliwi kwa minajili ya rangi bali uzao wa mtu; wanadamu walikuwa ni wanadamu na walijitambulisha kwa kundi la uzao wa baba zao ambao ni Japhet, Shem na Ham.

Japhet ambaye alikuwa ni mtoto wa kwanza wa Nuhu alizaa wana na wakajiita Wajapheti (Japhites), Shem akazaa wana nao wakajiita Washemu (Shemites), Ham naye akazaa watoto nao wakajiita Wahamu (Hamites). Daktari wa Historia Rudolf Windsor kwenye kitabu chake kinachoitwa "From Babylon to Timbuktu" katika Ukurasa wa 21 anasema miaka ya nyuma wanadamu walikuwa hawajitambulishi kwa kupitia rangi ya ngozi yao bali asili ya baba zao, hivyo haya mambo ya rangi yaliletwa na mwanasayansi mkubwa wa Ujerumani aitwae Johann Friedrich Blumenbach mnamo karne ya kumi na nane.

Johann aligawa makundi ya binadamu kwa kupitia rangi zao za miili, yote haya ilikuwa kutaka kusema kwamba watu weupe (Caucasian) ndiyo binadamu halisi. Hivyo akaseme duniani kuna jamii kuu tano ambazo ni Wazungu (Caucasian), Wamongolia (Mongoloid), Weusi (Ethiopoid) , Wamarekani (Red Indians) na Wahimalaya (Malayan). Hizi ndizo falsafa zilizoanza kuwagawa binadamu kwa kupia rangi zao kiasi cha kuwafanya watukuze ukoloni na mauji ya jamii yoyote tofauti na wao.

Wakati nasoma kuna kipindi tulipitia Falsafa karibia zote, kuanzia wakina Plato wa Ugiriki hadi wakina Frierich Nietzsche lakini falsafa za Wajerumani nyingi hazikuguswa. Falsafa ya Ujerumani ya kisiasa na Kisheria (German Historical and Political Jurisprudence) kwenye nchi nyingi za Ulaya na Marekani haiguswi kwasababu ndizo wakina Hitler na wanazi walizitumia kusema kwamba Ujerumani ni ya Wajerumani tu. Hivyo kutokana na kuwa na ushawishi hasi kwa jamii ya kibinadamu baada ya vita vya pili vya dunia falsafa hii ilianza kuyeyuka kidogo kidogo lakini kwa bahati mbaya Makabulu ambao wanahusiana na Wajerumani sana walikuja na ile falsafa na wakaianzisha nchini Afrika Kusini. Ndiyo falsafa hiyo hiyo iliyotumika na wakoloni wa kibelgiji nchini Rwanda-Urundi kwa kuwadanganya Watusi kwamba wao wako bora kuliko ndugu zao kwenye baadhi ya vitu na vizazi vingi baadae leo tunaona yaliyotoke mwaka 1994.

Je, huu mgawanyo wa Kisayansi ni sahihi?
Kwa mtizamo wangu jibu ni "Hapana" kwasababu siyo kila mweusi ni mwana wa Ham. Ikumbukwe kuna neno maarufu linalosema "Anti-Semitism" ambayo ni chuki dhidi ya Wayahudi lakini neno "Semite" halimaanishi Wayahudi pekee kwasababu neno hilo limetokana na makosa ya kimatamshi ya neno "Shemite" ambalo linamaanisha wazao wa Shem ambao siyo Wayahudi pekee. Hivyo basi ikumbukwe kuna Wayahudi weusi ambao siyo wana wa Ham, hawa wanaitwa Falasha Jews. Lakini kutokana na hiyo falsafa wale Wayahudi waliotoka Ulaya au Asheknazi Jew wanawadharau sana jamii ya Wayahudi weusi.

C: MGAWANYIKO WA VIZAZI: WAJUKUU WA NUHU.

Japheti ndiye anaaminika kuwa baba wa Wazungu kwasababu watoto wake ndiyo walikuwa wameenda kuishi sehemu za juu za Ulaya. Majina ya watoto wake ni haya yafuatayo:

  1. Javani ( Wagiriki, Warumi, Wahispania, Wareno,Waitalia na Wafaransa)
  2. Magog (Watu wa ukanda wa Ulaya Mashariki au Slaviki Region)
  3. Madai (Wahindi, Waajemi, Wakurdi,Wamedi, )
  4. Tubal (Jamii ya kusini mwa bahari nyeusi)
  5. Tira (Makabila na jamii za Kijerumani, waskandinavia)
  6. Mescheh (Warusi)
  7. Gomer ( Wakeltiki)
Shem ndiye baba wa watu wa jamii za Watu wanaoishi sehemu za Mashariki ya kati, kama Wayahudi na Waarabu. Na majina ya watoto wake ni haya yafuatayo:
  1. Elam ( Waarabu wa Saudi Arabia)
  2. Asshur (Waashuru)
  3. Lud (Walidia)
  4. Aram ( Wasiria)
  5. Arphaxad (Waebrania)
Ham ndiye baba wa watu weusi na aliishi sehemu za Mashariki ya Kati, Afrika na Ulaya Kusini karibu na Bahari nyeusi. Haya ya uwepo wa watu weusi huko yanasemwa na Mwanahistoria Herodotus ambaye alisema aliwaona Waethiopia wakiishi kwenye kando ya hiyo bahari. Na hata wamefukua mabaki ambayo inasemekana ni ya zaidi ya miaka 1000 Kabla ya Kristo na ni ya mtu mweusi. Basi wafuatao ndiyo watoto wa Ham:
  1. Mizraim (Misri)
  2. Kushi (Sudani na Ethiopia)
  3. Putu (Walibia na Makabila mengine ya Afrika)
  4. Canaan (Wahiti, Wayebusi, Waamori, Wasidoni, Waperizi n.k)

IKUMBUKWE: Jamii ya wanadamu tangu zamani za kale ilikuwa imechanganyikana sana hivyo kuna kipindi watu wa mashariki ya kati walikaa walikaa pamoja chini ya tawala mbali mbali, hivyo muingiliano ulikuwa mkubwa. Hakuna mwanadamu aisyekuwa na damu mchanganyiko katika dunia hii. Kama Waebrania walikaa utumwani Misri kwa miaka 400, Waafrika walitawala Hispania kwa zaidi ya miaka 800, Wakarthago walizaa na Waitalia watoto wengi baada ya Hanibbal kuvamia nchi yao hivyo wakawabaka sana wanawake wa kiitalia, Waajemi walitawala Misri kwa miaka mingi, Wagiriki walitawala Misri kwa miaka mingi sana na ndiyo wakatokea wakina Cleopatra: Na mfano ambao ni hai kabisa ni jinsi ambavyo machotara walitokea Zanzibar kipindi cha Usultani. Hivyo basi duniani nako kuna muingiliano mkubwa sana katika jamii.


CREDIT:Jamii Forums
JE WAJUA?:Mtu mweusi, "Kiumbe mwenye historia tata" JE WAJUA?:Mtu mweusi, "Kiumbe mwenye historia tata" Reviewed by Unknown on Januari 19, 2017 Rating: 5

Hakuna maoni

Post AD

Propellerads