Vikosi vya usalama vya Kenya vyawekwa katika hali ya tahadhari baada ya mauaji ya Baringo
Vikosi vya usalama vya Kenya vimewekwa katika hali ya tahadhari kaskazini magharibi mwa nchi hiyo baada ya kuongezeka mauaji katika Kaunti ya Baringo.
Manoah Esipisu, msemaji wa ikulu ya Rais ametangaza kuwa, hatua za kiusalama zimechukuliwa katika Kaunti ya Baringo baada ya kutokea machafuko katika eneo hilo. Aidha msemaji huyo wa Ikulu ya Rais amewataka viongozi wa Kaunti ya Baringo kuchukua hatua za kurejesha amani na utulivu katika eneo hilo na kutoingilia hatua na shughuli za kibinadamu.
Manoah Esipisu amesema pia kuwa, serikali haitawafumbia macho wanasiasa wanaowachochea watu kufanya machafuko.
Wakati huo huo, mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Kenya yamemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi Joseph Boinnet kupeleka vikosi zaidi katika Kaunti ya Baringo baada ya wanasiasa wawili kuuawa.
Katika upande mwingine Baraza la Magavana limemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuchukua hatua za kurejesha amani na uthabiti katika kaunti hiyo ya Baringo.
Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Peter Munya amesema kuwa, Joseph Nkaissery Waziri wa Mambo ya Ndani na Joseph Boinnet Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Kenya wanawaangusha Wakenya wakati ambao wanapaswa kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo kuwalinda raia.
Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya limetangaza kusimamisha shughuli zake za kibinadamu katika Kaunti ya Baringo baada ya mfanyakazi wake kushambuliwa siku ya Ijumaa.
Vikosi vya usalama vya Kenya vyawekwa katika hali ya tahadhari baada ya mauaji ya Baringo
Reviewed by Unknown
on
Februari 27, 2017
Rating:
Post a Comment