Header AD

NIKOHURU BLOG#Namna ya kukabili maumivu makali ya uti wa mgongo.

Maumivu yanayoanzia katika viungo vinavyotengeneza uti wa mgongo kutokana na uvimbe joto wa misuli, magegedu na pingili za mifupa, yanaweza kusambaa hadi
mapajani na wakati mwingine yanaweza kwenda hadi kwenye goti.
Maumivu yanayotokana na mgandamizo wa mizizi ya neva kutoka katika uti wa mgongo, husababisha maumivu ya miguu zaidi kuliko maumivu ya mgongo.
Maumivu hayo husambaa kwenye nyonga na mapajani hasa upande wa mbele. Maumivu yanaweza kujitokeza baada ya kutembea na mara nyingi huambatana na ganzi.
Kama maumivu ya mgongo yanatokana na kuachana kwa pingili za uti wa mgongo zilizokwenda upande, mara nyingi yanaongezeka pale mgonjwa anapokohoa, kupiga chafya au kuongeza msukumo wa tumbo wakati wa kujisaidia haja kubwa.
Mtu mwenye tatizo hili pia anaweza kushindwa kupata haja kubwa au kukojoa kutokana na mishipa ya fahamu inayopeleka habari katika utumbo au kibofu cha mkojo, kushindwa kufanya kazi sawasawa.
Hii ni kwa mujibu wa utafiti wa M.C. Jensen na wenzake uliochapishwa katika jarida la kitabibu lijulikanalo kwa jina la The New England Journal of Medicine toleo la 331(2) la mwaka 1994.

Uchunguzi na Matibabu
Kipimo cha X-ray kinaweza kuonyesha picha ya uti wa mgongo na kubainisha kama mifupa ya uti wa mgongo imevunjika au imeteguka.
Kipimo cha Computerized Tomography (CT scan) kinaweza kusaidia ili kuona matatizo yasiyoonekana kwa kutumia X-ray kama vile kuchanika kwa magegedu, kupungua kwa ukubwa wa tundu linalopitisha mishipa ya fahamu au kama kuna uvimbe unaokandamiza mishipa ya fahamu.
Kama maumivu ni ya muda mrefu, kipimo cha Magnetic Resonance Imaging (MRI) kinaweza kutumiwa.
Kipimo hiki kinaweza kuonyesha matatizo ya misuli, magegedu, mifupa na mishipa ya damu katika uti wa mgongo.
Kipimo hiki husaidia kubaini chanzo cha maumivu hasa wakati wa maambukizi, mteguko, uvimbe joto, uvimbe wa kawaida au uvimbe utokanao na saratani.
Kipimo cha Ultrasound (sonography) pia kinaweza kutumika katika uchunguzi wa tatizo la maumivu ya mgongo. Kipimo hiki kinaweza kuonyesha kama misuli ya uti wa mgongo imechanika.

Matibabu
Utafiti wa P.D. Roelofs na wenzake unaonyesha kuwa matumizi ya dawa za kupunguza maumivu na uvimbe joto ni nzuri kwa tiba ya muda mfupi ya tatizo hili.
Utafiti huo ulichapishwa mwaka 2008 katika Database ya Chochrane Systemic Reviews.
Wagonjwa wenye tatizo hili kwa muda mrefu wanaweza kupata msongo wa mawazo na sonona. Hawa wanaweza kutibiwa kwa dawa za kuondosha sonona pia.
Kukandakanda mgongo wa barafu au maji ya uvuguvugu pia husaidia kupunguza maumivu wakati matatizo haya yanapoanza.
Hii ni kwa mujibu wa Dk Brian A. Casazza, profesa mshiriki katika Kitivo cha Tiba za Mazoezi, Chuo Kikuu cha North Carolina Marekani, katika makala yake iliyochapishwa katika jarida la American Family Physician toleo la 85(4), 2012.
Matibabu kwa njia ya upasuaji pia yanaweza kufanyika pale chanzo cha tatizo kinapobainika kuwa ni uvimbe au mteguko unaogandamiza mishipa ya fahamu.
Njia nyingine ya kupunguza matibabu ni kufanyizwa mazoezi maalumu kulingana na mtaalamu atakavyopendekeza kulingana na eneo la uti wa mgongo, lililoathirika.

Jinsi ya kuzuia
Ni muhimu kula mlo kamili wenye viinilishe muhimu vinavyoimarisha afya ya mwili kwa ujumla.
Ni vizuri kujiepusha na utumiaji wa chumvi nyingi kwenye chakula na kuepuka matumizi ya pombe kupita kiasi ili kukwepa tatizo la kudhoofika kwa mifupa.
Ni vema pia kuachana na uvutaji wa sigara na matumizi mengine ya tumbaku kwani sumu zilizomo husababisha mishipa midogo inayopeleka damu mgongoni isinyae na kusababisha upungufu wa hewa ya oksijeni na viini lishe muhimu kwa ajili ya afya ya viungo hivyo.
Kufanya mazoezi ya mwili kama vile kutembea, kuogelea, kujinyoosha, kupiga pushapu na kukimbia ni muhimu ili kupunguza unene na maumivu ya misuli ya mgongo.
Wajawazito wanashauriwa kufanya mazoezi mepesi ya aina ya ‘Pelvic Rocking’ ambayo yanahusisha kuinama kwa kupiga magoti na kuweka viganja vya mikono chini huku akiinua mgongo juu taratibu.
Wanawake wanaovaa viatu vyenye kisigino virefu wanatakiwa kuchukua tahadhari hasa pale wanapolazimika kutembea muda mrefu.
Njia nyingine inayosaidia ni kukaa na kulala kwa namna inayofaa.
Ni vizuri pia kuepuka ubebaji wa vitu vizito kupita kiasi ili kuepuka matatizo yanayoweza kuumiza uti wa mgongo kwa namna moja ama nyingine.
Kwa ushauri kuhusu masuala ya afya>Madalali2007@yahoo.com

NIKOHURU BLOG#Namna ya kukabili maumivu makali ya uti wa mgongo. NIKOHURU BLOG#Namna ya kukabili maumivu makali ya uti wa mgongo. Reviewed by Unknown on Septemba 16, 2016 Rating: 5

Hakuna maoni

Post AD

Propellerads