Jaji Lubuva Ataka Tume ya Uchaguzi Ifumuliwe.......Apendekeza Wakurugenzi wa Halmashauri Wawekwe Kando Kwenye Usimamizi
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva ameitaka serikali kubadili muundo wa tume hiyo ili iwe na ofisi na watumishi katika kila halmashauri nchini na ofisi ya Zanzibar.
Amesema hatua hiyo itawezesha NEC kufanya kazi zake kwa uhuru zaidi, badala ya kutegemea wakurugenzi wa halmashauri (Ma-DED).
Alisema hayo jana mjini Dodoma wakati akikabidhi taarifa ya tathimini baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama.
Tathimini hiyo imetolewa ikiwa ni mwaka mmoja tangu Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli kutangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi huo.
Lubuva alisema serikali ifanyie mapitio ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 na Sheria ya Serikali za Mitaa Sura 292 ili kurekebisha vifungu vinavyokinzana.
“Pamoja na hayo, serikali inatakiwa kubadili muundo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili kuwa na ofisi na watumishi katika kila halmashauri nchini na ofisi ya Zanzibar, hiyo itafanya tume ifanye kazi zake kwa uhuru zaidi tofauti na sasa kazi hizo zimekuwa zikifanywa na wakurugenzi wa halmashauri,” alisema.
Alisema baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, tume iliamua kufanya tathimini kwa lengo la kupata mrejesho juu ya utekelezaji wa Uchaguzi Mkuu kutoka kwa wadau. Alisema ni mara ya kwanza kwa tume kufanya tathimini tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993.
“Tathimini hii imefanyika ikiwa ni mojawapo ya zoezi linalokamilisha mzunguko wa uchaguzi na kuanza kwa mchakato wa uchaguzi mwingine,” alisema.
Alisema changamoto zilizojitokeza kwa mujibu wa wadau waliohojiwa ni pamoja na mpiga kura kutoruhusiwa kupiga kura katika eneo tofauti na lile alilojiandikisha.
Pia wapiga kura kushindwa kupiga kura siku ya uchaguzi kutokana na kugawa mipaka ya kiutawala na majimbo ya uchaguzi, baada ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura na muda mfupi uliotolewa kujiandikisha na uwekaji wazi wa daftari la awali la wapiga kura.
Alisema tathimini inaonesha katika baadhi ya maeneo, watu waliojitokeza kupiga kura ni wachache, ukilinganisha na idadi ya wapiga kura waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
“Baadhi ya sababu zilizotolewa ni pamoja na uelewa mdogo juu ya umuhimu wa kupiga kura kutokana na elimu ya mpigakura kutowafikia wapigakura wengi, pia wapigakura walijiandikisha katika daftari la kudumu kwa ajili ya matumizi mengine ili kupata kadi kwa ajili ya matumizi mengine na uwepo wa hofu, vitisho na vurugu siku ya kupigakura,” alisema.
Waziri Mhagama, Mkurugenzi wanena
Kwa upande wake, Waziri Mhagama alisema tume inapaswa kupongezwa kwa kukamilisha zoezi zima la Uchaguzi Mkuu, ambalo lilikuwa na changamoto nyingi na ushindani mkubwa wa kisiasa.
Alisema kwa mujibu wa Kifungu cha 15(5) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura 343, tume inapaswa kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura mara mbili kati ya Uchaguzi Mkuu mmoja na mwingine, lakini haikuwezekana kufanyika hivyo baina ya mwaka 2010 na mwaka 2015 kutokana na sababu mbalimbali.
Alisema sababu hizo ni pamoja na ufinyu wa bajeti na kuchelewa kupatikana kwa fedha kwa wakati, lakini serikali itajitahidi kuhakikisha kuwa mapungufu yaliyo ndani ya uwezo wake, yanatatuliwa ili kuiwezesha tume kutekeleza majukumu yake ya kikatiba na kisheria kwa wakati.
Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima alisema tathimini ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ilifanyika, ikiwa ni hatua ya kukamilisha mzunguko wa uchaguzi.
Alisema kati ya watendaji 1,029 waliohojiwa, watendaji 929 ambao ni sawa na asilimia 90.3 walisema wana uelewa kuhusu muundo wa tume na watendaji 100 sawa na asilimia 9.7, walikuwa hawana uelewa kuhusu muundo wa tume.
“Kati ya watendaji 929 wa uchaguzi waliohojiwa, 818 sawa na asilimia 88 walisema kuwa muundo wa tume unafaa kuendesha uchaguzi, aidha watendaji 111 sawa na asilimia 12 walieleza kuwa muundo wa tume haufai katika kuendesha uchaguzi,” alisema.
Pia matokeo yanaonesha kuwa, katika watendaji wa uchaguzi 1,014 waliohojiwa, 814 sawa na asilimia 80.3 walisema hakukuwa na changamoto katika njia hizo, watendaji 200 sawa na asilimia 19.7 walieleza njia za mawasiliano zilikuwa na changamoto.
Alisema matokeo ya tathimini yameonesha kati ya watendaji 1,029 waliohojiwa 996 sawa na asilimia 96.8 walikuwa na maoni kuwa utekelezaji wa majukumu ya uchaguzi ulizingatia maelekezo yaliyotolewa na tume, ambapo watendaji 33 sawa na asilimia 3.2 walieleza kuwa utekelezaji haukuzingatia maelekezo hayo.
Aidha alisema wadau wa uchaguzi 1,915 waliohojiwa kuhusu uelewa wao juu ya elimu ya mpiga kura, kati ya wadau 1,463 sawa na asilimia 76.4 walisema walikuwa na uelewa wa elimu ya mpiga kura na 452 sawa na asilimia 23.6 hawakuwa na uelewa.
Kailima alisema wapiga kura 499 walihojiwa, ambapo kati yao wapiga kura 377 sawa na asilimia 75.6 walisema walitumia chini ya dakika 30 kufika kituo cha kupiga kura, wakati wapiga kura 87 sawa na asilimia 17.5 walitumia dakika 30 hadi 60 kufika kituo cha kupiga kura.
Jaji Lubuva Ataka Tume ya Uchaguzi Ifumuliwe.......Apendekeza Wakurugenzi wa Halmashauri Wawekwe Kando Kwenye Usimamizi
Reviewed by Unknown
on
Oktoba 29, 2016
Rating:
Post a Comment