Kauli ya Makamu wa Rais kufuatia mauaji ya watafiti wawili na dereva wao waliouawa kwa kuchomwa moto
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amelaani vikali mauaji ya watafiti wawili wa kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian cha Arusha na dereva mmoja waliokuwa kazini katika kijiji cha Mvumi Makulu, wilayani Chamwino mkoa wa Dodoma.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo jana tarehe 4-Oct-2016 wakati akifungua kongamano ya 30 la Kimataifa la Wanasayansi lililoandaliwa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais amesema kuwa tukio hilo ni baya na amewahakikishia watafiti wanaoshiriki kongamano hilo kuwa Serikali itachukua hatua stahiki kwa watu waliofanya kitendo hicho cha kinyama ili kukomesha tabia hiyo.
“Haiwezekani hata kidogo watu kufanya mauaji hayo ya kikatili na waachwe bila kuchukuliwa hatua kali za kisheria alisisitiza Makamu wa Rais”
Akizungumzia masuala ya utafiti, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali inatambua kazi nzuri inayofanywa na watafiti hao hivyo Serikali itaendelea kutoa mchango wake wa hali na mali ili kuhakikisha watafiti hao wanafanya kazi zao kwa ufanisi unaotakiwa.
Makamu wa Rais pia amewahimiza wafadhili waendelee kusaidia watafiti hasa wanaofanya tafiti za afya nchini kwa sababu tafiti hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa namna ya kukabiliana na magonjwa mbalimbali.
Amesema kuwa watafiti wanamchango mkubwa katika kuleta maendeleo kupitia matokeo ya tafiti zao nchini hivyo jitihada hizo ni muhimu zikaimarishwa ipasavyo.
Kongamano hilo la 30 la Kimataifa la Wanasayansi lililoandaliwa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu -NIMR- linajumuisha watafiti mbalimbali kutoka Ulaya, Afrika na Amerika.
Katika kongamano hilo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameshiriki katika zoezi utoaji wa tuzo kwa wanasayansi waliofanya tafiti mbalimbali za afya nchini.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es Salaam.
Kauli ya Makamu wa Rais kufuatia mauaji ya watafiti wawili na dereva wao waliouawa kwa kuchomwa moto
Reviewed by Unknown
on
Oktoba 05, 2016
Rating:
Post a Comment