Godbless Lema Aamua Kufunga Kula Akiwa Rumande
Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ameamua kufunga ili kuwa karibu na Mungu wakati akiendelea kushikiliwa na polisi mkoani Arusha.
Wakati Lema akiamua kufanya hivyo, taarifa zilizopatikana mjini Arusha zinaeleza kuwa polisi walikwenda naye nyumbani kwake kwa ajili ya upekuzi lakini hawakufanikiwa kupata chochote.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo na hata alipotafutwa kwa simu, hakupokea.
Suala la Lema kuacha kula ili awe karibu zaidi na Mungu lilielezwa na mwenyekiti wa Chadema wa mkoa, Amani Golugwa ambaye alisema ameelezwa na mke wa mbunge huyo.
Lema, ambaye alikamatwa Jumatano iliyopita mkoani Dodoma na kuletwa mjini hapa Alhamisi, bado hajafikishwa mahakamani. Imeelezwa kuwa viongozi wa chama chake wameshindwa kumuona kutokana na kuzuiwa na polisi.
Akizungumzia suala hilo jana, Golugwa alisema alipokea ujumbe kutoka kwa mke wa mbunge huyo, Neema Lema kuwa mumewe ameamua kufunga na kuomba kwa ajili ya Taifa kuhusu mambo yanayoendelea na kuwa ameona kipindi hiki ambacho yupo rumande ni cha kuwa karibu zaidi na Mungu.
“Kama tunavyomjua Lema ni mtu anayempenda sana Mungu, ameamua kujinyenyekeza mbele za Mungu. Anafunga na kuomba jioni mke wake anampelekea chakula na amesema yupo katika hali nzuri,”alisema Golugwa.
Golugwa alisema wamejitahidi kutaka kumuona Lema, lakini wamegonga mwamba na wameshindwa kumwekea dhamana mbunge huyo.
Alisema alizungumza na ofisa upelelezi wa makosa ya jinai mkoani hapa na Kamanda Mkumbo, wote walisisitiza kuwa Lema ataendelea kuhojiwa hadi watakapojiridhisha.
“Ni jambo la kushangaza kama mtuhumiwa anaweza kukaa rumande zaidi ya saa 48 kama sheria inavyotaka, nadhani hapa siyo sheria tena, labda ni kwa mujibu wa maelekezo ambayo hatujui yametoka wapi na kwa malengo yapi,” alisema Golugwa.
Alisema baada ya kuwasili kutoka Dodoma alifanikiwa kuonana naye mara moja tu na baadaye hakuna mtu aliyeruhusiwa kuonana naye; iwe viongozi wa Chadema au wakili wa chama hicho, John Mallya ambaye ameshawasili kwa ajili ya mambo ya kisheria .
Juzi, Kamanda Mkumbo alisema Lema hataachiwa hadi upelelezi ukamilike na mwanasheria wa Serikali atakapokuwa amemaliza kuandaa mashtaka kwa kuwa amekuwa akirudia makosa yaleyale ya uchochezi.
Godbless Lema Aamua Kufunga Kula Akiwa Rumande
Reviewed by Unknown
on
Novemba 06, 2016
Rating:
Post a Comment