Rais Magufuli atunuku Kamisheni kwa Maafisa Wapya wa JWTZ Ikulu Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli, jana tarehe 26 Novemba, 2016 ametunuku Kamisheni kwa Maafisa Wanafunzi 194 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kundi la 59/15 katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Hii ni mara ya kwanza kwa Maafisa Wanafunzi wa JWTZ kutunukiwa Kamisheni nje ya Chuo Cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli kilichopo mkoani Arusha, na ni mara ya kwanza kwa Maafisa Wanafunzi wa JWTZ kutunukiwa Kamisheni ndani ya Ikulu.
Maafisa hao ambao 168 ni wanaume na 26 ni wanawake, wametunukiwa Kamisheni katika cheo cha Luteni Usu na sasa wamekuwa Maafisa Wapya wa JWTZ.
Kabla ya kutunuku Kamisheni, Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli alikagua gwaride rasmi lililoandaliwa na Maafisa wanafunzi wa JWTZ na baadaye akashuhudia uhodari wa askari kutoka kikosi cha maadhimisho cha JWTZ waliofanya onesho la gwaride la kimyakimya.
Akizungumza baada ya chakula cha mchana katika ukumbi wa Ikulu, Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli alimpongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange, Makamanda na Askari wote wa JWTZ kwa jukumu kubwa wanalolitekeleza la kuhakikisha nchi ipo salama na amesema Serikali itahakikisha inaboresha zaidi maslai na mazingira ya kazi kwa Jeshi hilo na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
Aidha, Rais Magufuli alisema ameamua tukio hili la kutunuku Kamisheni lifanyike Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutoa heshima kwa Maafisa wa JWTZ kama ambavyo Viongozi wengine Serikalini wamekuwa wakipata heshima ya kuapishiwa Ikulu.
"Kwamba Mawaziri tunapotaka kuwaapisha tunawaapishia hapa, Wakuu wa Mikoa tunawaapishia hapahapa, Makatibu Wakuu tunawaapishia hapahapa, kwa nini hawa Maafisa wa Jeshi tusiwaapishie hapahapa kwenye nyumba yao? Nyinyi ndio mnalinda nchi, nyinyi ndio mnasimamia usalama wa nchi hii, lakini nikiuliza hapa inawezekana wengine mpaka wamekuwa Mabrigedia Jenerali hawajawahi kukanyaga Ikulu, wakati hapa ni kwenu"alisema Rais Magufuli.
Sherehe za kutunuku Kamisheni kwa Maafisa Wanafunzi hao zilihudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi na Wakuu wa Jeshi la Ulinzi wastaafu na Majenerali wastaafu wa JWTZ.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
Amiri Jeshi Mkuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akitunuku kamisheni kwa Maafisa Wanafunzi wa Kundi la 59/15 wa Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es salaam Novemba 26, 2016
Amiri Jeshi Mkuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akikagua gwaride la heshima linaloundwa na Maafisa Wanafunzi wa Kundi la 59/15 wa Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) kabla hajawatunuku kamisheni katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es salaam Novemba 26, 201.
Amiri Jeshi Mkuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akiweka saini kwenye hati ya kamisheni kwa Maafisa Wanafunzi wa Kundi la 59/15 wa Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) kabla hajawatunuku katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es salaam Novemba 26, 201
Amiri Jeshi Mkuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akiweka saini kwenye hati ya kamisheni kwa Maafisa Wanafunzi wa Kundi la 59/15 wa Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) kabla hajawatunuku katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es salaam Novemba 26, 201
Amiri Jeshi Mkuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akiongea baada ya kutunuku kamisheni kwa Maafisa Wanafunzi wa Kundi la 59/15 wa Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) katika ukumbi wa mikutano wa Ikulu jijini Dar es salaam Novemba 26, 201.
Amiri Jeshi Mkuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akiongea baada ya kutunuku kamisheni kwa Maafisa Wanafunzi wa Kundi la 59/15 wa Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) katika ukumbi wa mikutano wa Ikulu jijini Dar es salaam Novemba 26, 201
PICHA NA IKULU
Rais Magufuli atunuku Kamisheni kwa Maafisa Wapya wa JWTZ Ikulu Dar es Salaam
Reviewed by Unknown
on
Novemba 27, 2016
Rating:
Post a Comment