Header AD

Bawasiri (Haemorrhoids) inatibika kwa njia za kisayansi



Mmoja wa wasomaji wetu aliuliza: “Katika sehemu zangu za haja kubwa, kuna vivimbe kama vitatu na ninapata taabu kukaa. Nimetumia dawa aina ya Anusol lakini bado sijapata nafuu, je naweza kutibiwa kwa
njia gani za kisasa?” Msomaji mwingine nae anauliza: “Je dawa ya ugonjwa wa Bawasiri ni ipi hasa?”

Msomaji wetu mwingine pia anaeleza kuwa amesumbuliwa na maradhi ya Bawasiri kwa zaidi ya miaka kumi sasa na angependa kujua kama ugonjwa huu unatibika. Nae anauliza: “Je nitapata tiba ya ugonjwa huu?” Msomaji mwingine anamuelezea mchumba wake ana kinyama cha Bawasiri kimetoka katika njia ya haja kubwa na anauliza: “Je akienda hospitalini watakikata au atapewa dawa tu na kinyama kitatoka?”

Kutokana na maswali hayo na mengine mengi ambayo sikuyaandika hapa, nimeona kuwa ipo haja kwa siku ya leo tuangalie kwa kina jinsi maradhi haya yanavyotibiwa hospitalini kwa njia ya tiba zenye ushahidi wa kisayansi.

Kwanza kabisa ni vizuri kuelewa kuwa, kuna maradhi ya aina mbalimbali yanayotokea katika njia ya haja kubwa ambayo yanaweza kuwa na dalili zinazofanana na zile za maradhi ya bawasiri. Kwa sababu hiyo, ni vizuri kupata uchunguzi wa kitabibu kabla ya kuamua kuwa unaugua maradhi ya bawasiri.

Uchunguzi na vipimo
Kabla ya matibabu yoyote, daktari mwenye ujuzi wa tiba, atachunguza kwa kuangalia sehemu ya njia ya haja kubwa na kuona kwa macho hali halisi ilivyo. Baada ya hapo daktari anaweza kufanya kipimo kwa kutumia kidole cha shahada. Kidole hiki kikiwa ndani ya mpira wa kuvaa mikononi, kinaweza kulainishwa kwa vilainishi salama na kuingizwa katika njia ya puru ili kubaini hali ya uvimbe.

Daktari pia anaweza kutumia kipimo cha kutazama moja kwa moja katika njia ya haja kubwa kijulikanacho kwa jina la Proctoscopy au kipimo cha kutazama ndani ya utumbo mpana, Sigmoidoscope. Kipimo cha maabara cha kubaini damu iliyofichika; faecal occult blood test, nacho kinaweza kufanyika pale bawasiri daraja la kwanza inapokuwa ndani na inapokuwa vigumu kuibaini kwa kipimo cha kidole au proktoskopi.

Matibabu
Matibabu ya bawasiri kimsingi hutegemea dalili, hali na hatua ya ugonjwa. Kwa kawaida tiba ya awali ni kurekebisha mfumo wa maisha na mtindo wa kula. Mgonjwa hushauriwa kunywa maji mengi na kula vyakula vitakavyolainisha kinyesi kila siku. Vyakula hivyo ni kama vile matunda na mbogamboga kwa wingi, vyakula asili visivyo vya kukoboa, aepuke chumvi nyingi na pombe.

Mara nyingi mgonjwa hutibiwa kwa njia za kawaida zisizohusisha tiba kwa njia ya upasuaji. Mgonjwa mwenye kinyama au kivimbe kinachojitokeza nje, ataelekezwa jinsi ya kukalisha eneo la haja kubwa katika maji ya vuguvugu kwa muda wa dakika 15. Atatakiwa kufanya hivyo mara nyingi kadiri iwezekanavyo hasa kila baada ya kujisaidia.

Mgonjwa pia anaweza kupewa dawa za kupaka kwenye uvimbe ulioko katika njia ya haja kubwa au vidonge vya kuingiza ndani ya tundu la njia ya haja kubwa. Tiba hizi zitasaidia kupunguza uvimbe na maumivu anayoyapata mgonjwa wa bawasiri hasa wakati wa kujisaidia haja kubwa.

Kama maumivu yatazidi, tiba rahisi iitwayo ‘Rubber band ligation’ inaweza kufanyika kwa bawasiri iliyoko ndani ya puru, yaani pale mishipa inapokuwa haijajitokeza nje. Bawasiri daraja la kwanza na la pili. Hapa mishipa hufungwa na rubber band ili kuzuia damu kwenda kwenye eneo lililoathirika. Tiba nyingine ni ile ya kuunguza na kufunga uvimbe wa kinyama kwa kifaa maalumu (laser therapy).

Kama uvimbe wa mishipa ya vena ni mkubwa sana na unajitokeza sana nje ya puru (bawasiri daraja la 3 na 4), upasuaji unaweza kufanyika na hapa kinyama hukatwa na kuondolewa, kisha damu inayotoka hudhibitiwa kitaalamu. Tiba hii kitaalamu hujulikana kwa jina la haemorrhoidectomy.

Katika hospitali kubwa, aina nyingine ya upasuaji wa kisasa zaidi inaweza kufanyika pia. Tiba hii kwa jina la kitaalamu hujulikana kama Doppler-guided Haemorrhoidal Artery Ligation Operation (HALO) na wengine hupendelea kuiita Transanal Hemorrhoidal Dearterialization-Hemorrhoidectomy (THD).

Tiba hii ya upasuaji hufanyika bila kukata kinyama na bila kutumia dawa ya usingizi ingawa ganzi inatumika. Ni tiba ambayo haisababishi maumivu na mgonjwa anaweza kuendelea na shughuli zake baada ya saa 48 tokea kipindi cha kufanyiwa upasuaji.

Katika tiba hii, mishipa yote inayojitokeza nje, haikatwi bali inarudishwa ndani ya puru na kushonwa kwa nyuzi zinazoyeyuka zenyewe ili ijishikize kwenye misuli ya ndani ya haja kubwa na mishipa yote inayopeleka damu katika kinyama kinachovimba, hufungwa.

Lengo la kuifunga ni ili kuizuia isipeleke damu nyingi kwenye uvimbe. Baada ya hapo, sehemu hiyo hufunikwa kwa bendeji inayoyeyuka yenyewe baada ya kipindi fulani.

Dk Sushil Maslekar, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Magonjwa ya Njia ya Haja Kubwa katika Hospitali ya Spire Leeds nchini Uingereza, anasema kuwa tiba hii ni nzuri, haina madhara na inaondosha dalili zote za bawasiri kwa ufanisi mkubwa.

Utafiti wa miaka 10 wa Pravin J. Gupta na Surekha Kalaskar uliochapishwa mwaka 2008 katika jarida la sayansi za tiba liitwalo ‘Annals of Surgical Innovovation and Research’ toleo la 2(5), unabainisha kuwa upasuaji na kushona ngozi ya tundu la haja kubwa katika maeneo matatu ambayo kwa kawaida hutokeza bawasiri, unatoa matokeo mazuri zaidi ya uponaji wa bawasiri.

Pamoja na hayo yote, katika matibabu ya Bawasiri ni muhimu kukumbuka kuwa tiba hizi zinaponyesha lakini tatizo linaweza kujitokeza tena kama vyanzo vyake havikudhibitiwa. Ili kupona kabisa ni lazima mgonjwa arekebishe mfumo wake wa maisha na mtindo wa lishe.
Bawasiri (Haemorrhoids) inatibika kwa njia za kisayansi Bawasiri (Haemorrhoids) inatibika kwa njia za kisayansi Reviewed by Unknown on Januari 13, 2017 Rating: 5

Hakuna maoni

Post AD

Propellerads