Jitihada za Kuendelea Kuokoa Waliofukia Mgodini Zaendelea..!!!
Jitihada za kuwatafuta wachimbaji wadogo 14 wa mgodi wa dhahabu wa RZ uliopo Nyarugusu mkoani Geita waliofukiwa na kifusi baada ya udongo kuporomoka mpaka usiku zilikuwa zikiendelea.
Wachimbaji hao wamefukiwa kwenye shimo lenye urefu wa mita 38 walimokuwa wanachimba dhahabu .
Tukio la kuporomoka kwa shimo hilo lilitokea saa tisa usiku wa kuamkia jana na wachimbaji 13 raia wa Tanzania na mmoja mwenye asili ya China walikuwa ndani.
Akielezea tukio hilo, msemaji wa kampuni ya RZ, Francis Kiganga alisema shimo lililofukiwa na udongo licha ya kuwa na urefu wa mita 38 kwenda chini, pembeni lina njia yenye urefu wa mita nyingine 38.
Alisema sababu za udongo kuporomoka na kuziba njia ni eneo hilo kuwa na mashimo mengine yaliyochimbwa na wakoloni miaka ya 60 iliyopita na kusababisha udongo kutitia.
Mmoja wa wachimbaji aliyeshuhudia tukio hilo, Lucas Misalaba alisema saa nane usiku waliona shimo likititia ndipo walitoa taarifa kwa wenzao walioko chini kusogea na kukaa pembeni na baada ya muda kidogo shimo lote lilifukiwa na udongo.
Akizungumza baada ya kutembelea eneo hilo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Ezekiel Kyunga alisema yapo matumaini kwamba wachimbaji hao watakuwa hai na kuitaka idara ya madini mkoa kuongeza nguvu za uokoaji ili kuwanusuru wachimbaji hao.
Jitihada za Kuendelea Kuokoa Waliofukia Mgodini Zaendelea..!!!
Reviewed by Unknown
on
Januari 27, 2017
Rating:
Post a Comment