Header AD

Tarime: Mkurugenzi Awatumbua Watumishi Wawili....Aapa Kumuwajibisha Yeyote Ataripotiwa wa Utovu wa Maadili

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Elias Ntiruhungwa amewasimamisha kazi watumishi wawili wa halmashauri hiyo mbele ya kikao kwa madai ya kushindwa kufuata maadili ya kazi.

Waliosimamisha kazi ni, Jeveryson Kaguna kwa madai ya kushindwa kuandaa taarifa za watumishi kwa wakati zilizokuwa zinahitajika Ofisi ya Rais, zikiwamo za kupandisha madaraja na ongezeko la mishahara.

Mwingine aliyesimamishwa ni muuguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Tarime, Kegosa Nega kwa madai ya kuwatukana wagonjwa hospitalini, utoro kazini na ukaidi. 

Mkurugenzi huyo aliwasimamisha kazi katika kikao cha watumishi wa halmashauri alichokiitisha kwa ajili ya kuwakumbusha wajibu wao na kufuata maadili ya kazi.

“Kuanzia sasa ninamsimamisha kazi ofisa utumishi kwa uzembe wa kushindwa kuandaa taarifa iliyokuwa inahitajika Ofisi ya Rais mwezi uliopita. Tuliambiwa tuandae majina ya watumishi wanaotakiwa kupanda madaraja waongezewe mishahara na kueleza mahitaji ya watumishi.

“Lakini hajaandaa na nilikuwa namkazania kila mara sasa sijui kama watu watapandishwa madaraja maana muda umeisha taarifa hazijakwenda,” alisema.

Kuhusu kusimamishwa kazi kwa muuguzi, alisema alikaidi agizo la mkubwa wake wa kazi la kumsaidia mgonjwa aliyekuwa amebebwa kwenye kitanda kumsukuma kumpeleka wodini.

Alisema hospitali ya wilaya imekuwa ikilalamikiwa kuwa baadhi ya watumishi hutoa kauli chafu kwa wagonjwa na kupokea rushwa kutoka kwa wagonjwa. 

Alisema mtumishi yeyote atakayeripotiwa kwa vitendo vya uvunjifu wa maadili atamuwajibisha.

 “Mtu anakwenda kazini kwa muda anaotaka yeye halafu ni wa kwanza kutoka kazini,” alisema Ntiruhungwa. 

Mratibu Elimu Kata ya Nyamisangura, Emanuel Mwihechi alisema suala hilo la watumishi kupandishwa madaraja ni muhimu, lakini kwa halmashauri ya mji limekuwa ni kero kwa watumishi kucheleweshewa madaraja.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, John Marwa aliwataka watumishi wote wa Serikali kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia sheria na taratibu za kazi ili kuepuka matatizo yanayoweza kuzuilika.

Tarime: Mkurugenzi Awatumbua Watumishi Wawili....Aapa Kumuwajibisha Yeyote Ataripotiwa wa Utovu wa Maadili Tarime: Mkurugenzi Awatumbua Watumishi Wawili....Aapa Kumuwajibisha Yeyote Ataripotiwa wa Utovu wa Maadili Reviewed by Unknown on Januari 08, 2017 Rating: 5

Hakuna maoni

Post AD

Propellerads