Header AD

Waraka wa Zitto Kabwe kuhusu marudio ya Uchaguzi

Nachukua fursa hii kuwapongeza Sana kwa kazi kubwa mliyoifanya kwenye chaguzi ndogo za udiwani na ubunge zilizomalizika hivi punde nchi nzima. Ingawa hatukushinda hata kata moja katika kata 20 zilizokuwa zinashindaniwa, lakini tumefanya vizuri kwenye matokeo.

Chama chetu kilisimamisha wagombea katika Kata 5 kati ya Kata 20 nchi nzima, Isagehe (Kahama), Kijichi (Dar es salaam), Kiwanja cha Ndege (Morogoro), Nkome (Geita) na Tanga (Songea). Na pia tulisimamisha Mgombea katika Uchaguzi wa Ubunge Dimani (Zanzibar).

Baada ya kufanya kampeni kubwa mzunguko wa kwanza tuliweza kutazama na kuamua kuwekeza kwa nguvu kwenye Kata 3.

Pamoja na kuwa hatukushinda Udiwani wala Ubunge katika Uchaguzi , matokeo yameonyesha kukua kwa kasi kubwa kwa Chama chetu. Tukishika nafasi ya 2 katika Kata ya Isagehe (Halmashauri ya Mji wa Kahama) kwa kupata mara 2 ya Kura ya zile ambazo tulipata katika Uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, hali hiyo ipo pia katika Kata ya Kijichi jijini Dar es salaam na Nkome mkoani Geita.

Ni dhahiri kuwa sauti yetu imesikika, Kampeni zetu zilizojikita juu ya masuala ya wananchi zimeleta matunda kiasi.Nawapongeza sana viongozi wetu wa Chama katika Jimbo la Kahama Mjini kwa kazi kubwa tulioifanya na kupiga hatua kubwa. Nawaomba wasikate Tamaa bali wawekeze kwenye kuimarisha uongozi wa Chama Jimbo zima, kwenye kata zote ili kuwa tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Katika Kata za Nkome mkoani Geita na Kijichi mkoani Dar Es salaam tumefanya kazi kubwa Sana. Wagombea na viongozi wetu wa Chama wa mikoa hii na kata hizi wamepigana kwenye mazingira magumu sana ya ushindani mkali wa kisiasa. Kata hizi zimetupa fundisho kuwa wananchi wanataka ushirikiano wa vyama vya upinzani. Ujumbe huo umefika na nawaomba viongozi wetu wa Chama wajiandae kufanya kazi na vyama vingjne. Ubinafsi, roho mbaya, chuki na kukomoana hakuwezi kutusaidia. Lazima tubadilike sisi wenyewe kwanza kabla ya kutaka kuleta mabadiliko kwa wananchi.

Katika Kata ya Tanga Manispaa ya Songea na kata ya Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro wanachama wetu na viongozi walifanya kazi kubwa kuonyesha uwepo wa Chama kwenye maeneo yao. Wamepanda mbegu za Chama na kwa uwezo wa mungu mbegu hizi zitamea na kuzaa matunda.

Ni muhimu kukemea hali ya uchaguzi ya Dimani, Naibu Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano ya Umma – Zanzibar, ndugu Seif Hamad, ni miongoni mwa waliojeruhiwa kutokana na kipigo baada ya kutolewa Kituoni alipokuwa Wakala wa Chama kwa kupinga udanganyifu wa uchaguzi. Bado uchaguzi kwa upande wa Zanzibar hauendeshwi katika misingi ya haki na demokrasia.

Nawapongeza na kuwashukuru sana wanachama wote wa ACT Wazalendo mliojitoa kwa Hali na Mali kushiriki kampeni katika uchaguzi huu. Shukran za dhati Kabisa kwa madiwani wetu waliotumia gharama zao kwenda kuishi vijijini kutafuta kura za Chama chetu. Sina cha kuwalipa mungu atawalipa. Mmeonyesha mapenzi ya dhati kwa Chama chenu. Mmeonyesha uzalendo wa dhati kwa vitendo.

Nawapongeza viongozi wa Chama wote wakiwemo wale kwa Kitaifa kuanzia Mwenyekiti wetu – Mama Anna Elisha Mghwira, Makamu Mwenyekiti – Mzee Shaaban Mambo, Kaimu Katibu Mkuu – ndugu Said Sanani, na Naibu Katibu Mkuu – ndugu Msafiri Mtelemwa kwa kazi kubwa walioiafanya. Nawapongeza pia makatibu wa Kamati za Makao Makuu ya Chama kwa kuwa waratibu wa kata zilizoshiriki uchaguzi na kwa wale waliokuwa makao makuu kwa kufanya kazi kubwa ya kuwasadia wenzao waliokuwa kwenye mapambano. Kwa Kweli tumefanya kazi kama timu na sote tumechangia matokeo haya tuliyoyapata.

Uchaguzi umekwisha. Badala ya kutumia muda wetu kujadili matokeo, tukubali tumeshindwa na kuanza kujipanga kujenga Chama kwenye maeneo yetu. Tuwaunge mkono walioshinda lakini pia tuwakosoe wanaposhindwa kuwajibika. Tusiache kuwasemea wananchi na kuhangaika na changamoto zao za maisha – msingi wetu wa Siasa zinazojikita juu ya masuala ya wananchi ni muhimu sana.

Ndio kazi yetu hii Kama Chama cha siasa. Tulitumia fursa ya kampeni za chaguzi ndogo kupaza sauti kwenye masuala ya kitaifa na tulifanikiwa Sana kwenye masuala mbalimbali na kutengeneza ajenda za kitaifa. Tusichoke kuendelea kuwa Chama cha masuala na sio matukio. Chama cha hoja Badala ya viroja. Chama cha UTU.

Tuendelee kutaka shughuli za kisiasa kuendelea kwa mujibu wa Sheria. Tuendelee kulaani vikali uamuzi wa Serikali kuzuia vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara.

Ahsanteni Sana
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama (KC)
ACT Wazalendo

Januari 23, 2017
Waraka wa Zitto Kabwe kuhusu marudio ya Uchaguzi Waraka wa Zitto Kabwe kuhusu marudio ya Uchaguzi Reviewed by Unknown on Januari 24, 2017 Rating: 5

Hakuna maoni

Post AD

Propellerads