Bunge Lapitisha Muswada wa Sheria Kuwasaidia Wasio na Uwezo wa Kuwalipa Mawakili
Hatima ya wasaidizi wa kisheria pamoja na huduma ya msaada wa kisheria kwa watu wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za mawakili, sasa iko mikononi mwa Rais John Magufuli, baada ya Bunge kupitisha bila pingamizi Muswada wa Sheria ya Huduma ya Msaada wa Kisheria wa mwaka 2016.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe aliwasilisha muswada huo bungeni mjini Dodoma juzi wenye lengo la kuwa sheria itakayosimamia na kuratibu utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa watu wasiokuwa na uwezo, kuwatambua wasaidizi wa kisheria na mambo mengine yanayohusu utoaji wa msaada wa kisheria nchini.
Wakati akitoa majumuisho waziri huyo, alikubali kuufanyia marekebisho baadhi ya vifungu vya muswada huo baada ya kupokea maoni na ushauri kutoka kwa wabunge mbalimbali ikiwemo Kambi ya Upinzani.
Alisema muswada huo ukiwa sheria rasmi, utakuwa mkombozi kwa watanzania katika eneo la sheria, kwani wengi wao hawajui kusoma na kuandika, lakini pia wengi hawana uwezo wa kumudu gharama za kuajiri mawakili.
Alisisitiza kuwa sheria hiyo, itasaidia pia kupambana na kusaidia wale wote wanaoathirika na utekelezwaji wa mila na tamaduni potofu, zinazoendelea kutekelezwa nchini.
“Kuna mila na desturi zilizopitwa na wakati ambazo hazitambuliwi kisheria, lakini bado mila hizo zinatumika na kuumiza watu wengi sana kwa mfano masuala kama vile talaka, ndoa, watoto na mirathi haya ni mambo ambayo kupitia sheria hii yatakuwa na ahueni sasa,” alibainisha.
Alisema wananchi wengi wamekuwa wakikosa haki zao kisheria kutokana na kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya sheria; na mbaya zaidi sheria zilizopo, hazitambui kama mhusika ana uelewa gani wa kisheria.
Pamoja na kwamba, Dk Mwakyembe alichukua na kuyafanyia kazi baadhi ya maoni ya Kambi ya Upinzani, yaliyowasilishwa bungeni hapo juzi na Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Tundu Lissu, alikosoa namna mbunge huyo alivyotumia mifano ya Marekani katika suala zima la huduma ya msaada wa kisheria.
Alisema anasikitishwa na kitendo cha mbunge huyo, kuifanya Mahakama Kuu ya Marekani kuwa ni mfano wa kuigwa na Tanzania wakati mahakama hiyo ndio iliyokuwa inaongoza kwa muda mrefu tangu miaka ya 1800 hadi 1960 kukandamiza haki za watu weusi.
“Kwa muda mrefu kumekuwa watu humu ndani kazi yao ni ku google na kunukuu Kiingereza tu humu ndani bila kuangalia context. Kwa mfano kipindi alichotolea mfano mheshimiwa Lissu cha miaka 1800 kulikuwa na ubaguzi wa rangi wa kupindukia,” alisema.
Alisema mfano huo hauendani na hali halisi ya Tanzania, kwani nchi hiyo ilipata Uhuru tangu mwaka 1961 na kuanzia hapo, kila mtu akiwemo mhindi, mwarabu na mwafrika aliyepo nchini humo, alikuwa na uhuru hadi wa kupiga kura.
Alipendekeza wabunge kuhakikisha wanatumia mifano hai, inayoendana na hali halisi ya Tanzania ikiwa ni pamoja na kutolea mifano ya wazee na waasisi waliopo. “Wapo akina Mkwawa na kina Kinjekitile, hawa wamezungumzia mengi kuhusu masuala ya haki,” alisema.
Bunge Lapitisha Muswada wa Sheria Kuwasaidia Wasio na Uwezo wa Kuwalipa Mawakili
Reviewed by Unknown
on
Februari 02, 2017
Rating:
Post a Comment