TSNP kutinga kwa Dk. Ndalichako, wapanga kutoa tamko la kupinga vigezo vya kupewa mkopo
Mtandao wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Tanzania ( TSNP) umepanga kuunda kamati ya viongozi wa serikali za vyuo vikuu ili kukutana kwa dharura na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Joyce Ndalichako.
Pia imepanga kuandaa tamko la kupinga tamko la mabadiliko ya vigezo vitakavyozingatiwa katika utoaji mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, lililotolewa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Elimu Mhandisi Stella Manyanya.
Mtandao huo umedai kuwa, mabadiliko hayo ya vigezo yamesababisha wanafunzi wengi kukosa mikopo huku baadhi yao kupunguziwa fedha za kujikimu.
Mkurugenzi wa Haki za Wanafunzi TSNP, Venancy Shitindi jana alisemakuwa TSNP kwa sasa inakusanya taarifa za changamoto zinazo wakabili wanafunzi waliokosa mikopo ili kuandaa tamko la kupinga mabadiliko hayo, litakalo pelekwa katika Ofisi ya Rais, Waziri Mkuu na Wizara ya Elimu.
“Tumepanga kutengeneza kamati ndogo ya viongozi kwa ajili ya kukutana kwa dharura na waziri mwenye dhamana ya elimu ili kutoa malalamiko ya wanafunzi juu ya vigezo vipya vilivyotolewa na wizara yake, pia tunakusanya taarifa na kuandaa tamko tutakalolisambaza katika ofisi ya rais, wizara ya elimu na ofisi ya waziri mkuu,” alisema.
Alidai kuwa, mtandao huo umefanya utafiti wa vigezo vipya vilivyotajwa na kubaini kuwa haviendani na sera ya elimu ya mwaka 2014, wala ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) pamoja na mpango mkakati wa kitaifa wa maendeleo kama alivyosema Mhandisi Manyanya katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari.
“Baada ya kusoma taarifa ya Naibu Waziri Manyanya tulikwenda kuangalia sera ya elimu ya mwaka 2014, tukakuta hakuna sehemu iliyoainisha kundi linalostahili kupata mkopo bali imeeleza elimu itolewe bure na mikopo itolewe kwa kila mwanafunzi. Na kwamba elimu imepewa kipaumbele cha kuleta maendeleo katika nyanja zote haijasema kwa wanaosomea masomo ya sayansi pekee,” alisema na kuongeza.
“Hata mpango wa maendeleo wa miaka 5 yaani 2025, unaeleza kuwa Tanzania inatakiwa kuwa na uchumi wa kati na kwamba imetoa kipaumbele elimu kutolewa bure kwa nyanja zote ili wapatikane wataalamu wa fani mbalimbali na wa kutosha.”
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Mhandisi Manyanya ilisema kuwa serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, huandaa sifa na vigezo vya utoaji Mikopo kila mwaka ili kuendana na malengo na matarajio yaliyopo katika mipango na mikakati ya kitaifa kama ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa 2025.
Na kwamba Serikali imetoa vipaumbele katika utoaji mikopo kwa wanafunzi wa mafunzo ya Fani za Sayansi za Tiba na Afya,Ualimu wa Sayansi na Hisabati, Uhandisi wa Viwanda, Kilimo, Mifugo, Mafuta na Gesi Asilia, Sayansi Asilia na Mabadiliko ya Tabianchi, Sayansi za Ardhi, Usanifu Majengo na Miundombinu.
TSNP kutinga kwa Dk. Ndalichako, wapanga kutoa tamko la kupinga vigezo vya kupewa mkopo
Reviewed by Unknown
on
Oktoba 21, 2016
Rating:
Post a Comment