Chadema Kukata Rufaa Hukumu ya Mbunge Aliyefungwa Jela Miezi Sita
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema hakikubaliani na hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Kilombero dhidi ya Mbunge, Peter Lijualikali na kwamba imepanga kukataa rufaa katika Mahakama Kuu.
Lijualikali ambaye ni Mbunge wa Kilombero, alihukumiwa kwenda jela miezi sita baada ya mahakama kumtia hatiani kwa kosa la kufanya fujo na kusababisha taharuki na uvunjifu wa amani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Makao Makuu ya chama hicho yaliyopo Kinondoni, Dar es Salaam, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema Lijualikali ni mfungwa wa kisiasa na amefungwa kwa sababu ya vita ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Upinzani.
Lissu alisema, wanachokifanya ni kukataa rufaa Mahakama Kuu na kisha kupeleka maombi ya dhamana mahakamani ili mbunge huyo apate dhamana wakati rufaa yake ikisikilizwa.
Aliongeza kuwa taarifa ya kusudio la kukata rufaa imeshapelekwa mahakama ya wilaya ili kuharakishiwa kupewa nakala ya mwenendo wa kesi na hukumu kwa ajili ya kukata rufaa hiyo.
“Sisi kama chama tunaamini kwamba mheshimiwa Lijualikali ni mfungwa wa kisiasa. Kesi iliyofunguliwa dhidi yake ilikuwa ya kisiasa ili kutekeleza malengo ya kisiasa ya CCM dhidi ya Chadema na hata adhabu yake imetolewa kwa sababu za kisiasa,” Lissu.
Alisema wamekuwa wakimuandama mbunge huyo tangu akiwa diwani na kwamba walimshitaki mara mbili wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana ili wamfunge lakini walishindwa na mbunge huyo alishinda uchaguzi.
Lissu alisema kutokana na kumkosa katika kesi walizomfungulia ndio sababu ya kumfunga miezi sita bila faini, wakiamini kuwa wanaweza kumuondolea ubunge wake aliopewa na wananchi wa Kilombero waliomchagulia.
“Timu ya wanasheria wa chama imeshaanza taratibu za kukata rufaa, kwa kuandaa notisi ya rufaa na maombi ya dhamana ya dharura wakati uamuzi juu ya rufaa yake unasubiriwa. Tunatazamia kukamilisha taratibu hizi hadi kufikia Jumatatu ijayo,” alisema.
Lissu aliongeza kuwa viongozi, wanachama na wafuasi wa Chadema katika jimbo la Kilombero, hawatakiwi kuwa na wasiwasi kwa kuwa adhabu hiyo haina athari zozote kwa hadhi yake kama mbunge.
Alifafanua kuwa Katiba iko wazi kwamba katika kifungu cha 67 (20) (c) kinaeleza kuwa mtu hatakuwa na sifa ya kuwa mbunge “…ikiwa mtu huyo amehukumiwa na Mahakama yoyote katika Jamhuri ya Muungano na kupewa adhabu … ya kufungwa gerezani kwa muda unaozidi miezi sita kwa kukutwa na hatia ya kosa lolote, vyovyote linavyoitwa, linaloambatana na utovu wa uaminifu.”
Adhabu ya kifungo aliyopewa Lijualikali haijazidi miezi sita. Katika hatua nyingine, Lissu alisema kesho akiambatana na Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe wataenda kumtembelea Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ambaye yuko katika Gereza la Kisongo mjini huo.
Alisema baada ya kumtembelea Lema watazungumza na vyombo vya habari kwa ajili ya kupaza sauti ili haki ya mbunge huyo aweze kuachiwa kwa kuwa wanaamini naye ni mfungwa wa kisiasa kama alivyo Lijualikali
Chadema Kukata Rufaa Hukumu ya Mbunge Aliyefungwa Jela Miezi Sita
Reviewed by Unknown
on
Januari 13, 2017
Rating:
Post a Comment