Mahakama ya Kisutu yamtaka Mhe.Tundu Lissu kufika mahakamani kujieleza kwa nini asifutiwe dhamana.
Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imemtaka mbunge wa Singida Mashariki kupitia CHADEMA, Mhe.Tundu Lissu anayekabiliwa na kesi ya uchochezi pamoja na wahariri wa gazeti la Mawio kufika mahakamani kujieleza kwa nini asifutiwe dhamana.
Hakimu Simba ametoa agizo hilo jana baada ya Lissu pamoja na mdhamini wake kutokuwepo mahakamani hapo kama sheria inavyotaka na hatua hiyo ilifikiwa baada ya wakili wa serikali kuomba itolewe hati ya kumkamata lakini hakimu Simba akamtaka Lissu aende kujieleza kwanini asifutiwe dhamana.
Katika kesi hiyo ya uchochezi, hakimu Simba alitoa uamuzi ambao umeuruhusu upande wa mashtaka kuyaleta upya mashtaka yanayofanana na yale yaliyoondolewa awali mahakamani hapo kutokana na kutokuwa na kibali cha mkurugenzi wa mashtaka (DPP) kwa kuwa ya sasa yanakibali na kuyatupilia mbali maombi ya Kibatala.
Hakimu Simba alisema upande wa mashtaka walikuwa na haki ya kurekebisha mapungufu na kuyaleta tena mashtaka hayo mahakamani.
Baada ya uamuzi huo kutolewa wakili Peter Kibatala alidai kuwa hawajaridhika na uamuzi huo watakata rufaa kuupinga kwa sababu wanaamini mashtaka hayo yalivyofutwa ilikuwa na maana ya kuwa yamekufa na akaiomba mahakama kutoyasoma mashtaka hayo mapya hadi rufaa yao itakaposikilizwa na mahakama kuu na kutolewa uamuzi.
Wakili wa serikali mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekwisha kamilika.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti hilo, Simon Mkina, Jabir Idrisa na mchapishaji wa kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob ambao awali walikuwa wakikabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na sheria ya magazeti ya mwaka 2002.
Chanzo: ITV
Mahakama ya Kisutu yamtaka Mhe.Tundu Lissu kufika mahakamani kujieleza kwa nini asifutiwe dhamana.
Reviewed by Unknown
on
Septemba 21, 2016
Rating:
Post a Comment