Header AD

CCM Waigomea CUF Zanzibar.....Wasema Hawako Tayari Kujadili Uchaguzi Mkuu 2015


\
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar  kimesema hakina mpango wa kufanya mazungumzo au makubaliano na Chama Cha Wananchi (CUF) kuhusiana na suala la Uchaguzi uliopita.

Msimamo huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alipokuwa akijibu hoja zilizotolewa na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF Ismail Jussa Ladhu katika Mahojiano Maalum na Gazeti moja hapa nchini Juzi.

Alisema  Uchaguzi umekwisha kazi iliyokuwepo mbele ya CCM ni kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho ya mwaka 2015/2020 ili kuhakikisha ahadi zilizotolewa katika kampeni za uchaguzi mkuu na viongozi wa CCM zinatekelezwa kwa vitendo.

Vuai alieleza kwamba kupitia  Mazungumzo na Gazeti la NIPASHE JumaPili Octobar  9, mwaka huu, Jussa alinukuliwa akisema  CUF inaangalia uwezekano wa kufanya mazungumzo na CCM kuhusiana na suala la uchaguzi, jambo ambalo CCM haipo tayari kukaa meza moja na Chama hicho kujadili jambo ambalo lishafanyiwa uamzi halili kwa mujibu wa kanuzi,taratibu na Sheria za nchi.

Alisema  Chama hicho kinaweza kukikaribisha Chama chochote cha upinzani kufanya mazungumzo juu ya namna gani ya kuimarisha na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM na siyo suala la Uchaguzi Mkuu kwani umepita kisheria na serikali zinaendelea kuwatumikia wananchi kwa uadilifu.

Alisema kitendo cha kujadili  serikali zote mbili ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  kwa sasa ni kwenda kinyume na Sheria za nchini kwani  serikali hizo zimetokana na maamuzi halali ya wananchi kupitia mfumo wa Uchaguzi wa kidemokrasia.

Aliwataka wafuasi wa Chama hicho na Wananchi kwa ujumla kupuuza  madai yaliyotolewa na Kiongozi huyo hasa mantiki ya kuundwa kwa serikali ya mpito Zanzibar , hatua ambayo haiwezekani na inaashiria kuvunja Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984.

“CCM hatuna mpango wa kukaa meza moja na Chama chochote cha upinzani na sio CUF tu, kujadili Uchaguzi kwani tayari umepita kwa vigezo vyote vya uhalali wa kisheria.

"Pia Hoja na Ajenda  ya kufanyika kwa Uchaguzi wa Mpito Zanzibar  kwa sasa ni ndoto za mchana ama kujifurahisha kwa kutafuta umaarufu wa kisiasa usiokuwa na uzani wala  mafanikio kwa wafuasi wa Chama kinachojenga hoja hizo hapa nchini.”, alisema Vuai na kuongeza kuwa CCM inaamini kwamba Uchaguzi umekwisha na sasa inajipanga na maandalizi ya Uchaguzi ujao wa mwaka 2020.

Naibu Katibu Mkuu huyo, alifafanua kwamba CUF kwa sasa imekosa muelekeo ndiyo maana viongozi wake wanafikia hatua ya kuwadanganya wafuasi wao kwa mambo ambayo kiuhalisia wanajua kuwa hayawezekani kufanyika katika historia ya uwanja wa kisiasa Zanzibar.

Alisema Chama cha kisiasa chochote pamoja na kuwa na jukumu la kushinda na kusimamisha Dola katika uchaguzi mkuu bado kinatakiwa kuwa na miongozo imara ya kusimamia ukweli, haki na uwazi kwa wafuasi na wananchi, vigezo ambavyo vimekosekana ndani ya CUF toka kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Alisisitiza kwamba kazi iliyopo mbele ya Chama hicho ni pamoja na kujiandaa kwa mambo mbali mbali yakiwemo Uchaguzi wa ndani wa CCM wa mwaka 2017, kwa ajili ya kupata viongozi makini na mahodari ambao pia watakuwa na jukumu la kusimamia maandalizi ya uchaguzi wa mwaka 2020.

Alilitaja jukumu la msingi linalotekelezwa na chama hicho ni pamoja na uhakiki wa Mali za CCM ili kujiridhisha zaidi ikiwa ni mkakati wa uimarishaji hali ya siasa na uchumi ndani ya CCM.

Aliwasihi  wafuasi wa Chama hicho na wananchi kwa ujumla kuendelea kuwa watulivu na kushirikiana kikamilifu na serikali zote mbili Serikali ya Awamu ya saba ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya awamu ya Tano ya  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .

Aidha aliwataka wananchi kuwafichua baadhi ya wanasiasa wanaojihusisha na vitendo vya kuharibu amani na utulivu wa nchi.

CCM Waigomea CUF Zanzibar.....Wasema Hawako Tayari Kujadili Uchaguzi Mkuu 2015 CCM Waigomea CUF Zanzibar.....Wasema Hawako Tayari Kujadili Uchaguzi Mkuu 2015 Reviewed by Unknown on Oktoba 11, 2016 Rating: 5

Hakuna maoni

Post AD

Propellerads