(AFYA MHIMU) Haya ndiyo Mambo ya kuzingatia kabla ya kuwa mjamzito
UJAUZITO ni safari ndefu inayomchukua mwanamke miezi tisa au majuma arobaini hadi kujifungua. Ni safari yenye mikikimikiki na hatari nyingi kwa mama na mtoto. Tusichukulie suala la ujauzito kama jambo la kawaida ingawa pia ni wajibu kwa mwanamke. Ujauzito siyo hali ya hatari au kutisha endapo mambo ya msingi yatazingatiwa kabla ya kuwa mjamzito na kipindi cha ujauzito hadi baada kujifungua.
Katika kipindi cha ujauzito kuna mambo mengi ambayo ni mabadiliko humtokea mama na mtoto aliye tumboni.
NINI CHA KUFANYA KATIKA KIPINDI HIKI?
Ni vyema upange sasa unataka kuwa mjamzito au mwezi fulani unataka kushika mimba, uwe na mpango. Hata hivyo, hakikisha umri wako upo zaidi ya miaka 20 kwa usalama zaidi wa afya yako. Mshirikishe mwenzi wako na mwambie ungependa upate ujauzito, siyo vizuri kushtukiza kwani inaweza kukupa ‘stress’ wewe mwenyewe au mwenzako endapo mmoja wenu hajajiandaa kisaikolojia.
CHEKI AFYA YAKO
Hakikisha una afya njema, huna magonjwa sugu kama kisukari, shinikizo la damu, magonjwa mengine ya moyo, kansa, HIV, kifafa, pumu, siko seli au grupu lako la damu ni RH Negative.
Endapo una matatizo haya hapo juu, basi haraka wasiliana na daktari wako wa masuala ya uzazi akupe ushauri kwani magonjwa mengine yatakusumbua wakati wa ujauzito, au magonjwa yenyewe yatamwathiri mtoto.
Hakikisha huna magonjwa au matatizo katika viungo vya uzazi, mfano kutokwa na uchafu ukeni wenye muwasho na harufu mbaya, vipele au vidonda sehemu za siri, maumivu wakati wa tendo la ndoa, kutokwa na damu au usaha ukeni. Vile vile mfumo wako wa uzazi uwe vizuri, matatizo katika mfumo wa uzazi ni kama vile maumivu ya tumbo chini ya kitovu, kuvurugika kwa mzunguko wa hedhi, kutopevusha mayai na kukosa hamu ya tendo la ndoa.
ACHA VILEVI
Epuka unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara, hili hata kwa mwanaume anayetaka mtoto. Mwanamke kabla ya kuwa mjamzito hakikisha unakula sana mboga za majani ili upate kiwango kizuri cha vitamin ya Folic Acid, ni vema ule sana mboga za majani au upate virutubisho vya Folic Acid. Endapo hutakuwa na kiwango kizuri cha Folic Acid, kuna hatari ya kuzaa watoto wenye matatizo.
MAZOEZI
Fanya mazoezi mepesi mara kwa mara ili kuimarisha nyonga na viungo vyako vingine na usipate matatizo wakati wa kujifungua. Pata ushauri wa daktari kipindi muafaka.
(AFYA MHIMU) Haya ndiyo Mambo ya kuzingatia kabla ya kuwa mjamzito
Reviewed by Unknown
on
Desemba 02, 2016
Rating:
Post a Comment