Watu 20 wafariki kutokana na baridi kali Ulaya
Watu zaidi ya 20 wamefariki kutokana na baridi kali ambayo imeendelea kukumba maeneo mengi ya Ulaya.
Miili ya wahamiaji watatu, wawili kutoka Iraq na mmoja kutoka Somalia, ilipatikana karibu na mpaka wa Uturuki na Bulgaria.
Vifo pia vimeripotiwa Italia, Jamhuri ya Czech na Ukraine.
Safari nyingi za ndege pia zimesitishwa kutokana na hali mbaya ya hewa.
Nchini Uturuki, mlango wa bahari wa Bosphorus umefungwa na meli haziruhusiwi kupita kutokana na dhoruba kali ya theluji.
Nchini Serbia, safari zote za mashua katika mto Danube zimesitishwa.
Viwango vya joto katika baadhi ya maeneo ya Urusi vimeshuka hadi nyuzi joto -40C (-40F).
Ugiriki, ambayo kawaida huwa haishuhudii majira mabaya zaidi ya baridi, viwango vya joto maeneo ya kaskazini vimefikia -15C (5F). Katika maeneo hayo, mhamiaji kutoka Afghanistan alifariki kutokana na baridi wiki iliyopita. Barabara katika eneo hilo zimefungwa.
Mjini Athens, kiwango cha joto kilikosa kupita 0C mwishoni mwa wiki, na visiwa vingi eneo hilo vimefunikwa na theluji.
Baadhi ya visiwa vya Ugirini vimekuwa makao ya maelfu ya wahamiaji ambao sasa wanahamishiwa makao mapya ya muda au mahema yenye mitambo ya kuongeza joto.
Majumba zinaowahudumia watu wasio na makao nchini Italia sasa yanafunguliwa usiku na mchana kuwahudumia watu wasio na makao.
Watu watano kati ya saba waliofariki nchini humo walikuwa watu wasiokuwa na makao.
Viwanja vya ndege Sicily, Bari na Brindisi vilifungwa mwishoni mwa wiki.
Hali pia si nzuri mjini Roma.
Na nchini Urusi, Moscow kulikuwa na baridi kali zaidi katika kipindi cha miaka 120 siku ya Krismasi ya kanisa la Orthodox tarehe 7 Januari.
Safari za ndege zilifutwa au kuahirishwa mjini Moscow.
Shule katika baadhi ya maeneo zilifungwa Jumatatu, ingawa maafisa wanasema hali itaimarika siku chache zijazo.
Mji wa Prague katika Jamhuri ya Czech ulipata usiku wa baridi kali zaidi usiku wa kuamkia leo. Watu watatu walifariki, wawili kati yao wakiwa watu wasiokuwa na makao.
Nchini Poland, watu 10 walifariki Jumapili na sasa maafisa wanasema idadi ya waliofariki kutokana na baridi tangu tarehe 1 Novemba wamefikia 65.
Miji ya Warsaw na Krakow ilitangaza Jumatatu kwamba wachukuzi wangeruhusiwa kusafiri bila kulipa nauli.
Watu 20 wafariki kutokana na baridi kali Ulaya
Reviewed by Unknown
on
Januari 10, 2017
Rating:
Post a Comment